Mkuu wa Mkoa wa rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amezishauri taasisi za kidini nchini kuhakikisha wanaangalia fursa za kuwekeza kwenye viwanda ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Amesema kuwa taasisi za kidini zimejitahidi sana kuisaidia serikali katika kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu na afya kwa kujenga mashule na vituo vya afya, lakini imefika wakati kuanza kufikiria fursa zilizopo katika uwekezaji wa viwanda.
“Tutafurahi sana tukisikia kuwa kuna viwanda vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini, Kama vile Mvinyo si lazima kuagiza kutoka nje ya Mkoa kama rasilimali zinapatikana hapa, Ngozi zinatyupwa lakini viwanda vya Ngozi hakuna, halafu ukienda dukani unaulizia kama kiatu kimetengenezwa kwa “pure leather”, naomba tuunge Mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano,” Amesema.
Ametoa ushauri huo alipokuwa akitoa salamu kwenye Jubilei ya miaka 50 ya parokia ya Mtakatifu Epifania jimbo la Sumbawanga ambapo mgeni rasmi wa sherehe hizo alikuwa Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga Mhashamu Baba Askofu Damian Kyaruzi.
Na kuongeza kuwa waumini wakiungana kwa nia hiyo, wanaweza kufanya maajabu na kuanzisha kiwanda katika Mkoa.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi wa sherehe hizo Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga Mhashamu Baba Askofu Damian Kyaruzi alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa nasaha zake na kupitia miradi mbalimbali ambayo kanisa inaifanya katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.
“Tunashukuru Mh. Mkuu wa Mkoa kwa kupitia miradi yetu, tunafanya shughuli za kijamii za elimu na afya kwa kujenga mashule na mahospitali, na kwa nasaha zako umetupa nguvu na tutakuja ofisini kwako bila ya taarifa.” Alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa