Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna mstaafu Zelote Stephe amesikitishwa na kitendo cha halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuwa na hoja za kujibu zipatazo 60 ambazo zimesababisha halmashauri hiyo kupata hati ya mashaka wakati halmashauri hiyo imeajiri watumishi wenye uwezo wa kuepusha jambo hilo lisijitokeze.
Akizungumza katika kikao cha baraza la dharula la madiwani Jana Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa anasikitishwa sana na kitendo hicho kwani wataalamu hao wameajiriwa huku serikali ikiwa inamatumaini kuwa ni watu wenye uwezo sasa zinapotokea hoja hizo yeye binafsi zinamsikitisha sana.
Alisema kuwa halmashauri hiyo haipaswi kuwa na huruma na watu wote waliosababisha hoja hizo kwani wanaoumia ni wananchi kutokana na baadhi ya watendaji kusababisha hali hiyo ambayo inapelekea halmashauri kupata hati ya mashaka na hata chafu na yeye akiwa ni Mkuu wa mkoa hatakubaliana na hilo.
"Binafsi nachukizwa sana na hali hii, siipendi hata kidogo kwani inaumiza na kuonekana hatuna watendaji wenyeuwezo, abadani sitakubali hali hii katika mkoa wangu labda uwe mkoa mwingine," Alisema.
Aliongeza kuwa madiwani wanapaswa Kutambua kuwa wao ndio taa ya halmashauri, kwani wakilegalega na halmashauri ikiendelea kupata hati ya mashaka wajue watakwenda kujibu wenyewe kwa wananchi ambao wamewatuma kuwawakilisha ili kuleta maendeleo katika halmashauri.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh.Kalolo Ntila alisema kuwa hoja hizo hazikutokana na baraza lililopo hivi sasa, na hata Mkurugenzi aliyopo hivi sasa na kuahidi kuwa wale wote waliosabaisha hoja hizo lazima watafutwe popote waliopo na kuchukuliwa hatua.
" hatutawaacha watu hawa bali tunazipitia hoja moja baada ya nyingine na kuzitolea majibu,lakini zile ambazo kitakuwa na matatizo ni lazima waliopo sababu sha wasakwe popote walipo na hatua dhidi yao zichukuliwe" alisema
Awali akizungumza katika baraza hilo la madiwani Mkaguzi mkazi na mdhibiti wa hesabu za serikali John Nalwambwa alisema kuwa ofisi yake ilibaini kuwepo kwa hoja 60 zenye utata ambapo hoja 25 kati ya hizo ndizo zilizopelekea kupata hati ya mashaka.
Alisema kuwa kuna fedha zaidi ya shilingi milioni 40 ambazo hazieleweki vizuri matumizi yake na baadhi ya vitabu vya makusavyo vikiwa vimepotea na hivyo nilazima ifahamike hatma ya suala hilo.
Alisema kuwa ofisi yake imefanya kazi kwa weledi mkubwa bila kuonea mtu na ndiyo imebaini hayo hivyo basi ni jukumu la halmashauri kuona ni jinsi gani itajibu hoja hizo ili zisijirudie tena.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa