Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen amewasisitiza madiwani kufuatilia miradi, kusimamia mapato na utawala bora ili Halmashauri za mkoa wa Rukwa ziweze kuendelea na kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Aliyasisitiza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na Manispaa ya Sumbawanga zote za Mkoa wa Rukwa siku ya tarehe 15 Mei, 2017. Mafunzo yanayoendeshwa na mradi wa PS3 unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la watu wa Marekani USAID.
Katika kuyafafanua kila jambo Mh. Zelote alianza kwa kuwasisitiza waheshimiwa Madiwani Kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi yote inayotekelezwa na Halmashauri zetu.
Mh. Zelote aliwakumbusha fedha zinazotoka Serikali kuu na kupelekwa Serikali za Mitaa na kutumika katika utekelezaji wa miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo, Elimu, Afya, Maji, Barabara namengineyo. Hivyo aliwasisitiza kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora unaotarajiwa.
“Nimekuwa nikifanya ziara nyingi sana katika kata mbalimbali zenye miradi hii, na nikifika huko naona namna miradi hiyo inavyotekelezwa chini ya viwango mpaka huwa najiuliza hivi kuna diwani kweli kwenye kata hii, mbona miradi hii ambayo ni faida kwa wananchi inakuwa haieleweki?” Mh. Zelote alieleza.
Kwa upande wa kusimamia mapato Mh. Zelote aliwatahadharisha madiwani hao kuwa kama Halmashauri haitakusanya mapato ya kutosha maana yake Halmashauri haitakuwepo jambo litakalopelekea wananchi kukosa huduma muhimu na kucheleweshewa maendeleo.
“Watumishi wote katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wafanye kazi kwa juhudi na maarifa na pia waepuke kufanya kazi kwa mazoea ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato, na Wakurugenzi wa halmashauri zote wasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato,” Mh. Zelote alisisitiza.
Katika kuhakikisha madiwani wanaelewa maana ya utawala bora katika kupeleka maendeleo kwa wananchi Mh. Zelote alisisitiza kuwa maendeleo hayana vyama, dini, ukabila na kwamba wadau wote wa maendelo wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili wananchi wote wapate maendeleo kwa usawa.
Mkuu wa Mkoa alisema, “Ili wananchi wawe ni sehemu ya maendeleo ya miradi inayopelekwa katika maeneo yao basi waheshimiwa madiwani ndio madaraja ya kupeleka maendeleo hayo, hivyo wao wanatakiwa kuwa kitu kimoja na kuachana na itikadi za kisiasa ili kuwafikishia wananchi maendeleo.”
Katika kukazia yale aliyoyazungumza Mh. Zelote aliwaomba madiwani hao kuyatumia vizuri mafunzo hayo yaliyotolewa na mradi wa Public Sector Strengthening System (PS3) na kuwashukuru watu wa Marekani ambao kwa kupitia shirika lao la Maendeleo USAID wameweza kufadhili mafunzo hayo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa