Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna mstaafu Zelote Stephen amempa masaa 24 Mkuu wa Wilaya ya Kalambo kuhakikisha vifaa vya huduma za Afya vilivyorundikwa katika zahanati ya Kasanga anavitawanya na kuanza kutumika katika zahanati hiyo na nyinginezo ili kusaidia upungufu wa vitanda uliopo kwenye zahanati hizo.
Alitoa agizo hilo baada ya kuvikuta vitanda vitano, magodoro matano pamoja na mashuka kumi ya hospitali yakiwa yamehifadhiwa kwenye store ya dawa ya zahanati hiyo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hali halisi ya iwepo wa madawa na huduma zinazopatikana katika zahanati hiyo inayohudumia wananchi zaidi ya 2000.
Vifaa hivyo ni miongoni mwa Vitanda 16 vyakuzalishia, Vitanda 80 vya Wagonjwa, Magodoro 80, na Mashuka 200 vilivyotolwa kwa Mkoa wa Rukwa ambavyo alivigawa Mh. Zelote tangu tarehe 27/7/2017 kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli aliyetoa vifaa hivyo kwenye halmashauri zote nchini ili kusaidia upungufu wa vifaa hivyo kwenye vituo vya afya na zahanati na kuboresha huduma za afya nchini.
“Mh. Rais hakutoa vifaa hivi ili vije kukaa kwenye stoo wakati kuna wananchi huko wanalala chini, mpaka kufikia kesho nitaagiza gari ije kuvibeba ili vikatumike kwa zahanati zenye shida zaidi maana ninyi hamna shida,” Mh. Zelote Alisema.
Pamoja na hayo Mh. Zelote aligundua kuwa Zahanati hiyo haina Mganga na baada ya kuhoji alijibiwa kuwa Mganga wa Hospitali hiyo yupo masomoni na tangu mwezi wa sita mwaka huu ameanza mitihani yake hali ambayo ilimstaajabisha Mh. Zelote na kuahidi kulishughulikia jambo hilo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa