Mkuu wa Mkoa wa Rukwa KamishnamStaafu Zelote Stephen amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri ya Sumbawanga vijiji na Manispaa kuhakikisha wanamalizia ujenzi wa barabara ya Mollo - Songambele Azimio kabala ya Msimu wa Mvua kuanza.
Ametoa agizo hilo baada ya kutembelea katika kijiji hicho kuona maendeleo ya miti aliyoshiriki kuipanda pamoja na wanakijiji hao katika maadhimisho ya siku ya kupanda miti kimkoa tarehe 19/1/2017 ambapo siku hiyo aliahidi kuwajengea barabara hiyo.
"Wakurugenzi nataka kabla ya Mvua kunyesha barabara hiyo iwe tayari, Mkurugenzi wa Sumbawanga Vijiji kwakuwa wewe umesema kipande chako ni kidogo sana basi ukimaliza kesho nitafurahi sana." Alisema.
Nao kwa upande wao kila mmoja baada ya kupewa nafasi Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Suumbawanga Saad Mtambule alisema kuwa barabara hiyo imeshaanza matengenezo kwa kiwango cha changarawe na kuwa inaendelea vizuri.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini Nyangi Msema Kweli aliahidi kuwa ahizo hilo litatekelezwa kwani tangu ahadi itolewe mwanzoni mwa mwaka huu, halmashauri ilishaiweka barabara hiyo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 na kuwaahidi kuwa pesa ipo ya kufanaya matengenezo hayo.
msisitizo huo uliibuka baada ya Diwani wa Msanda muungano Mh. Charles Kanoni kuanza kufanya mikutano na kuwaambia wananchi kuwa barabara hiyo haitatengenezwa kakuwa haikuwa kwenye bajeti yoyote ya halmashauri ya Sumbawanga Vijijini jambo ambalo lilimshtua Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule.
Dk. Haule alisisitiza kuwa alitegemea diwani kuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo na badala yake anakuwa kinyume na matarajio ya wanakijiji na kumuonya kutojihusisha na kusema uongo kwa wananchi ili ajitengenezee ulaji na kuongeza kuwa serikali ya awamu hii inatekeleza ahadi zake zote na hakuna ahadi itakayotolewa ambayo haitatekelezwa.
Ziara hiyo ilikuwa maalum kwaajili ya kuhamasisha upandaji wa miti katika kijiji hicho ili kiwe cha mfano katika Wilaya na Mkoa wa Ujumla juu ya upandaji wa Miti.
Aidha, Mh. Zelote pia aliahidi kukisaidia kikundi cha ngoma cha Mwalimu Nyerere cha kijiji hicho kuimarisha vifaa vyao na hatimae kuendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kujiongezea kipato katika shughuli zao za kila siku.
"Kama nilivyoahidi nilipokuja mwanzoni mwa mwaka huu leo hii nimetoa shilingi 167000 kwa kikundi hiki ili waboreshe vifaa vyao vya kazi," RC alisema.
Na kuwaomba wadau mbalimbali wa utamaduni kujitokeza kusaidia kuuinua utamaduni wa wafipa na wa mkoa kwa ujumla.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa