Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ametoa siku 15 kwa waajiri wote waliotowa ahadi hewa kwa wanyakazi kuhakikishe wanawalipa wafanyakazi hao ili kutoa motisha kwa wengine kwa miaka inayofuata.
Alitoa agizo hilo alipokuwa akiwahutubia watumishi wa taasisi mbalimbali za kiserikali na mashirika ya Umma katika viwanja vya Namanyere wilayani Nkasi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani.
Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila ifikapo Tarehe 1, Mei ya kila mwaka na kusheherkewa na wafanyakazi wote wa serikali na mashirik binafsi Duniani na wafanyakazi waliofanya vizuri huzawadiwa kwa kupewa pesa Taslimu, hundi ama vifaa mbali mbali ili kuongeza ushindani kwa wafanyakazi.
Mh. Zelote alisema “Endapo wapo watumishi bora ambao hawajalipwa nataka nipate majina yao mara moja, vinginevyo ifikapo tarehe 15 Mei, 2017 wawe wamelipwa,” na kuongeza kuwa katika mchakato wa kupatika kwa wafanyakazi bora chama cha Wafanyakazi Tanzania TUCTA kishirikishwe na waajiri hao.
Pamoja na hilo Mh. Zelote Stephen alisisitiza kufanyika kwa mabaraza ya kazi kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza ili kila mfanyakazi ajue haki yake na aidha aliwashauri wale ambao wanategemea kustaafu kuhakikishe wanawasilisha nyaraka zao muhimu ili taratibu za mafao zikamilike kwa muda muafaka.
“Hata hivyo yanapotokea matatizo ya kuzungushwa taarifa ziletwe kwangu mara moja ili hatua zinazostahili zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kushughulika na mwajiri mzembe,” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa