Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen ametoa siku saba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Kalambo pamoja na Mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) kumpatia orodha kamili ya vyombo vyote vya majini vinavyofanya shughuli zake katika mwambao wa ziwa Tanganyika katika Wilaya za Nkasi na Kalmbo za Mkoa wa Rukwa.
Ametoa agizo hilo alipotembelea mwambao wa Ziwa Tanganyika katika Kijiji cha Wampembe, Kata ya Wampembe Wilaya ya Nkasi na kubaini mitumbwi kadhaa iliyokuwa ikizagaa kwenye mwambao huo ikiwa haijafanyiwa usajili na kusababisha upotevu wa mapato ya serikali kupitia sekta hiyo ya uvuvi.
“Halmashauri zimekuwa zikilalamika hazina mapato ya kutosha wakati naona pesa zikielea tu hapa na Hakuna chochote kinachoendelea, sasa natoa siku saba kwa Halmashauri na SUMATRA nipate orodha kamili ya vyombo vyote vya usafiri wa majini, usajili wao na leseni zao zinazowaruhusu kufanya shughuli za uvuvi katika mwambao huo.” Amesema.
Pamoja na hayo agizo hilo pia limekuja baada ya wiki moja iliyopita boti ambayo mmiliki wake hakujulikani kuzama ziwa Tanganyika ikitokea katika Kijiji cha Kalila, Kata ya kabwe, tarafa ya Kirando, Wilayani Nkasi kuelekea Kijiji cha Kyala Mkoani Kigoma na kupelekea kifo cha mtoto mmoja na watoto wengine wawili kuhofiwa kufa maji huku watu 11 wakiokolewa. Na wafanyakazi wawili wa boti hiyo kukimbia.
Katika kuhakikisha usalama wa Kijiji cha Wampembe unaimarika Mh. Zelote aliagiza kuhamishwa kwa watumishi wawili, Afisa Mtendaji wa kata ya Wampembe Faustine Wakulichamba pamoja na Afisa uvuvi wa Kata Godfrey Kashengebi kwa makosa mbalimbali moja ikiwa kutosimamia makusanyo ya mapato ya uvuvi jambo lililopelekea kudorora kwa makusanyo ya mapato pamoja na kuwepo kwenye kata hiyo kwa miaka zaidi ya sita jambo ambalo linapunguza ufanisi wao wa kazi.
Katika doria hiyo Mh. Zelote pia alikamata kokoro na nyavu kadhaa zilizokuwa hazikukidhi vipimo vya serikali katika matumizi yake jambo ambalo maafisa hao walifumbia macho na kuisababishia serikali upotevu wa mapato.
Kwa mujibu wa sheria za halmashauri mtumbwi wenye urefu wa mita 4 hulipiwa dola 4 kwa mwaka kama ada ya usajili.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa