Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameipa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi siku tatu kuhakikisha kuwa wanafanya marekebisho ya mfumo wa maji unaohudumia kituo cha afya cha Wampembe jambo ambalo linakwamisha huduma ya maji katika kituo hicho.
Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya ghafla katika kituo hicho ili kuona utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa tangu kuanza kwa mwaka huu, ziara hiyo ya siku tatu ililenga kuangalia utekelezaji katika sekta ya elimu, afya, maji, na uwekezaji wa viwanda.
Katika kuhakikisha jambo hilo linakamilika aliagiza mhandisi wa maji wa Halmashauri hiyo Eric Namakonde ambaye aliambatana na msafara huo kubaki siku hizo na kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika na kupatiwa ripoti.
“Nimekuja mwezi wa tano na kuagiza hili jambo likamilike mpaka sasa sioni kinachoendelea, huwa sipendi kurudia maagizo sasa mhandisi wa maji ubaki hapa hadi marekebisho yakamilike na taarifa inifikie mezani ndani ya siku tatu,” Amesema
Kijiji cha Wampembe kipo mwambao wa Ziwa Tanganyika, Wilaya ya Nkasi na kutoka makao makuu ya wilaya hadi katika Kijijini hapo ni kilomita 117 umbali ambao unasababisha hali mbaya kwa wananchi ambao wanataka kufanyiwa upasuaji katika kituo hicho ambacho kina maabara iliyokamilika ila inakosa huduma ya maji tu, na gharama ya marekebisho ya uharibifu Shilingi 800,000/=.
“Msafara huu ambao nimekuja nao, si ushafikia hiyo gharama tayari, sasa mnataka tuwe tunakuja huku kila siku kwaajili ya jambo hili tu, sasa sitaki kurudi huku kwa jambo hili tena,” Amesema.
kwa muda wa miaka miwili wananchi wamekuwa wakilazimika kuchota maji katika visima vilivyopo Kijiji hapo na kufikisha kituoni hapo pindi ndugu yao anapotaka kufanyiwa upasuaji jambo ambalo Mh. Zelote hakukubaliana nalo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa