Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza kusitishwa ujenzi wa kiwanda cha unga katika eneo la jirani na zahanati ya Kilimahewa kata ya Malangali wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mh. Wangabo ametoa agizo hilo baada ya kupokea kero za wananchi aliporuhusu maswali katika Mkutano uliofanyika Malangali sokoni, baada ya mkazi wa eneo hilo Raymond Mwanazyumi kuhoji sababu za kiwanda hicho kendelea kujengwa karibu na zahanati wakati waliugomea ujenzi huo.
“Uwekezaji na hospitali amabyo itakuwa inahusu kelele vitaoana kweli, watu watashindwa kulala na hao wagonjwa si wataugua mara mbili, hoja ya msingi kuna eneo limetengwa la uwekezaji hajaanza kujenga hajapewa kibali cha kuendeleza ujenzi kwahiyo asiendeleze hapo mahali,” Alisisitiza.
Kufuatia malalamiko hayo Mh. Wangabo alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu kutoa majibu ya madai hayo. Nae alisema kuwa mwekezaji huyo wa Kampuni ya London Agro Factor inayomilikiwa na Asayile Masaku alizuiwa kuendelea na ujenzi huo kwa kuwa eneo hilo si rafiki kwa ujenzi wa viwanda.
Amesema taarifa alizonazo ni kwamba mwekezaji huyo yupo katika mchakato wa kutaka kubadili matumizi ya eneo hilo kutoka kuwa la viwanda hadi kuwa la makazi.
"Tunahitaji wawekezaji na tumetenga maeneo ya viwanda. Hili eneo ambalo Masaku anataka kujenga kiwanda cha unga analimiliki kihalali lakini lipo kwa ajili ya makazi ya watu, tulimwambia tupo tayari kumpa kiwanja eneo maalum la uwekezaji Kanondo” amesema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa