Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amechangia shilingi milioni moja kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kusaidia ujenzi wa kituo cha afya cha Waislamu kinachoendelea kujengwa katika Tarafa ya Kirando, Kata ya Kirando Wilayani Nkasi.
Amesema kuwa Taasisi za kidini kwa muda mrefu zimekuwa zikisaidia juhudi za serikali katika kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi jambo ambalo pia linasaidia utekelezaji wa Ilani ya chama tawala inayoongoza serikali hiyo.
“Naendelea kuzishukuru taasisi za kidini kwa kuisaidia serikali katika kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinawafikia wananchi kwani kwa uopande wa sekta ya Afya Mkoa una zahanati kumi, vituo vya afya vinane na Hospitali mbili zinazomilikiwa na taasisi za kidini na mmeniambia kuwa mnaendelea na ujenzi wa vituo viwili vya afya ambavyo vikikamilika vitaongeza upatikanaji wa huduma,” Alielezea Mh. Wangabo.
Ametoa mchango huo kuzindua harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya katika siku ya maadhimisho ya mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika Kimkoa katika Kijiji cha Kabwe, Kata ya Kabwe Wilayani Nkasi ambapo Mgeni rasmi wa shughuli hiyo alikuwa Mh. Joachim Wangabo.
Pia aliwashukuru waumini hao kwa kuendelea kuiombea serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na watendaji wote na kusisitiza kuendeleza maombi hayo ikiwemo na kuhubiri amani iliyopo ili nchi isonge mbele katika sekta zote.
Nae katibu wa BAKWATA Mkoa wa Rukwa Mohammed Khatibu alipokuwa akisoma risala mbele ya mgeni rasmi alisema kuwa Baraza hilo linahitaji kiasi cha shilingi 6,910,000 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya ambacho kipo katika hatua ya upauaji.
“Tunaendelea na ujenzi wa kituo cha afya kilichopo kirando Nkasi ambacho kwa sasa kipo katika hatua ya kupauliwa na mahitaji yetu kwa sasa ni kupata bati za futi 8 bando 11 zenye thamani ya shilingi 2,970,000/= mbao za kenchi 500 zenye thamni ya shilingi 5,000,000/= fundi pamoja na misumari, thamani ya jumla ni shilingi 6,910,000/=” Alifafanua
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa