Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali mkoani wa Rukwa ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya tanounaosimamiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema kuwa huduma za kijamii zikiwemo afya na elimu zimeendelea kuimarika na kuongeza kuwa hadi sasa serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 zilizotumika kujenga na kukarabati vituo vya afya 9 pamoja na kutenga shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya kuanza ujenzi wa hospitali za wilaya huku katika ngazi ya vijiji serikali imejenga zahanati mpya 19 na nyingine 60 zikiendelea kumaliziwa.
Kwa upande wa elimu Mh. Wangabo amesema kuwa uandikishaji wa darasa la kwanza umeongezeka kwa asilimia 26 toka mwaka 2015 na idadi ya shule zenye kidato cha tano zimeongezeka kutoka shule 10 mwaka 2016 hadi shule 15 mwaka 2018, hii ni sawa na ongezeko la asilimia 50.
“Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha madawati yanatengenezwa mashuleni. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2015/2016 tulikuwa na madawati 37,311 kwa shule za msingi, meza 21,757 na viti 22,093 kwa shule za Sekondari. Aidha, kwa mwaka 2018 madawati yameongezeka kufikia 80,501 kwa shule za msingi, meza na viti 33,686 kwa sekondari kufikia mwaka huu 2018.”Alisema.
Kwa upande wa upatikanaji wa maji katika mkoa wa Rukwa umeongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 53.3 mwaka 2018 huku serikali ikitenga shilingi bilioni 5.6 kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 kwaajili ya kuendelea na ujenzi wa miradi ya maji na kampeni ya usafi wa mazingira mkoani Rukwa.
Aidha, pato la mwanachi katika Mkoa limeongezeka kutoka shilingi 3,714,792 kwa mwaka 2016 hadi kufikia shilingi 4,064,393 mwaka 2017 kwa mujibu wa takwimu za mwezi April, 2018 kutoka ofisi ya takwimu (NBS)
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa