Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo ameendelea kuwatahadharisha wananchi wa mkoa huo juu ya uwepo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid – 19) na kuwataka kuendelea kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kufuata maelekezo yote ya wataalamu wa afya.
Aidha, amesisitiza kuendelea kujifukiza kwa kutumia majani yaliyoelekezwa na wataalamu, majani ambayo yanapatikana kwa wingi sana katika mkoa wa Rukwa na kuwaasa kutoona aibu kwani njia hizo zimekubaliwa na kiutambuliwa na taasisi za afya nchini pamoja na kurtumika na viongozi mbali mbali wa ngazi za juu nchini.
“Watu wanaambiana kwamba ugonjwa umeisha, haujaisha, ugonjwa wa Covid – 19 bado upo, na sisi mkoa wa Rukwa tumepata wagonjwa pia, wengine wamepona wengine bado, kwahiyo chukueni tahadhari, ugonjwa bado upo na Mheshimiwa Rais wetu kipenzi cha watanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amekwisha tahadharisha pia kwamba ugonjwa huu upo, ila tumshukuru Mwenyezi mungu sana kwasababu ukali wa ugonjwa huu sio kama ilivyotokea kule Marekani, Hispania, Italy na kwingineko, tuna unafuu mkubwa sana kwahiyo tumshukuru Mwenyezi mungu kwa jambo hili,” Alisema.
Halikadhalika aliwataka wananchi hao kuendelea kutumia nyumba za ibada kufanya maombi na kuwasihi kuendelea vyombo vya kunawia katika nyumba hizo za ibada pamoja na kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko hiyo huku akieleza umuhimu wa barakoa kuwa ni kubaki na vimelea vyako wakati wa kukohoa ama kupiga chafya ili visisambae kwa wengine na kuwaletea madhara.
“Umuhimu wake ni kwamba mimi ninapoongea kama hivi, tunapopeana mita mbili tatu, tunapoongea mate yanatoka, yanapotoka yaishie kwenye barakoa, ndio maana tunazivaa, hatuvai kama vile mapambo na kuwa tumeelekezwa tu tuvae, hapana, lakini pia unazuia pale ambapo mwenzako anaongea yale mate yake yasikufikie wewe, ni lazima tutumie barakoa ili kuhakikisha kwamba maambuki haya yasikufikie wewe ama yasimfikie mwenzako kama wewe unayo bila ya kufahamu,” Alitahadharisha.
Pia alieleza kuwa endapo mtu atapatwa na dalili za ugonjwa huo ambazo ni homa kali, vidonda vya kooni, mwili kuchoka, na kukohoa mara kwa mara akimbilie katika kituo cha kutolea huduma za afya ili ajue hali yake na kuchukua hatua stahiki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa