Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasifu wananchi wa kata ya Mtowisa, Tarafa ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga kwa kuonyesha mshikamano katika ujenzi wa shule ya Sekondari Vuma pamoja na ujenzi unaonendelea wa kituo cha polisi kitakachohudumia tarafa ya mtowisa.
Tarafa hiyo yenye kata 4 ina shule moja ya kidato cha tano na sita jambo alilosifu Mh. Wangabo kuwa imetimiza ilani cha Chama Tawala kwa kuwa na Shule moja ya aina hiyo kwa kila tarafa.
Amesema kuwa ataendelea kusisitiza kauli ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa maendeleo hayana vyama, hivyo alisisitiza wananchi hao kutobaguana kwa itikadi zao bali wahimizane katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo katika tarafa yao.
“Mmenivuti mliponieleza kwamba mnashirikiana katika nyanja mbalimbali, kuna majengo yale ya shule mnashirikiana na jengo hili la polisi mnashirikiana ili kuhakikisha kwamba changamoto mbalimbali zilizopo ndani yenu mnazitatua, hili limenifurahisha na ningependa muendelee nalo, na umeoja na mshikamano uliopo muudumishe bila ya kujali vyama vyenu.” Alisifu.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha mtowisa, kata ya mtowisa Wilayani Sumbawanga katika ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali na kujitambulisha kwa wananchi.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya mtowisa Mh. Edgar Malini alisema kuwa wananchi wa mtowisa hawana tabu wa kutoa ushirikiano ili kujiletea maendeleo wenyewe isipokuwa wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu umeme na maji.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa