Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameipongeza Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Rukwa kwa kuvuka kiwango walichopangiwa kukusanya kwa mwaka wa fedha 2019/2020 pamoja na nusu yam waka wa fedha 2020/2021 huku akitoa maagizo kwa Wakurugenzi ambao mapato yao ya ndani bado yanasuasua.
Mh. Wangabo amesema kuwa mapato yatokanayo na kodi na vyanzo vingine ndio yanayotegemewa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati nchini ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR, mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Miundombinu ya barabara, Elimu, Afya, Maji na mengineyo na hivyo kuwaomba wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati na kuwasisitiza kila wanunuapo wadai risiti.
“Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mkoa wa Rukwa ulipangiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 13.78 kupitia TRA Hata hivyo, tulifanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 14.56 sawa na 106% na mwaka wa fedha 2020/2021 kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba, 2020, Mkoa wa Rukwa ulipangiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 5.23. Hata hivyo, tumefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5.61 sawa na 107%, Haya ni mafanikio mazuri, hivyo TRA iendelee kufanya bidii zaidi katika kazi yao ya ukusanyaji wa mapato.”
Aidha ametoa maagizo kwa wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kuweka nguvu kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani Pamoja na kudhibiti kikamilifu matumizi ya fedha za Halmshauri ili kuwaletea maendeleo wananchi kwa wakati na kwa kuzingatia bajeti na mipango yao.
“Kwa Mwaka huu wa Fedha wa 2020/21, Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zilikisia kukusanya shilingi 9,487,289,000.00 Hata hivyo, Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Julai, 2020 hadi tarehe 22 Disemba, 2020 Halmashauri zimekusanya kiasi cha shilingi 3,682,531,918.16 sawa na asilimia 38.8 ambapo zilipewa kukusanya angalau asilimia 50.” Alisisitiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika salamu zake za Krismasi na Mwaka Mpya wa 2021 kwa wananchi wa mkoa wa huo na kuongeza kuwa Katika kipindi cha kuanzia tarehe 1.7.2020 hadi 22.12.2020 Halmashauri ya Manispaa ya sumbawanga imekusanya asilimia 41.3, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imekusanya asilimia 40.6, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo imekusanya asilimia 39.9 na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imekusanya asilimia 33.8
Katika kipindi cha mwaka ujao wa 2021 Serikali ya Mkoa itajielekeza zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi mbalimbali bila shuruti. Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ni lazima sasa iwe rafiki wa mlipa kodi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa