Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Katibu tawala wa Mkoa Bernard Makali kuitisha kikao maalum cha wataalamu wa kilimo kutoka katika Halmashauri zote Mkoani humo ili kubaini mahitaji sahihi ya mbolea kwa manufaa ya sasa nay a baadaye.
Amesema kuwa wataalamu wanaelewa kiasi cha mbolea inayohitajika kulingana na hekta za zilizopo katika Mkoa kwa kukokotoa hesabu na kupata jibu sahihi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili takwimu hizo zifanane.
“Katibu Tawala itisha kikao cha wataalamu wote wa kilimo kutoka katika Halmashauri zote, mkae mtafakari na kuja na takwimu sahihi, takwimu zikitupotosha tunapotea wote hata serikali inapotea kwasababu tunaweza kuagiza kiasi kikubwa mno na kupoteza pesa nyingi kumbe mahitaji ni kidogo, na ndio maana kunakuwa na sense hata za watu ili watu wapange mambo yao vizuri, kwenye Kilimo kuna lega leg asana,” Ameeleza.
Amesema kuwa walio wengi wanafanya kazi kwa ubabaishaji ambao unaonekana kwenye takwimu ambapo hapo awali ilionekana kuwepo na uhitaji wa tani 97,000 tofauti na takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwepo kwa uhitaji wa tani 27,000 ambapo kati ya hizo tani 11,000 tayari zimepatikana ikiwa tani 5,000 za UREA na tani 6,000 za DAP jambo mabalo haliendani na uhalisia maana uhitaji wa mbolea kwa sasa sio mkubwa baada ya tani hizo kufika kulinganisha na tani tunazozisubiri.
Katika kuhakikisha idara hiyo inafanya kazi yake kwa ufanisi Mh. Wangabo amesema kuwa aliyekuwa akikaimu ukuu wa Idara hiyo katika ofisi yake amewekwa pembeni na kumpisha kaimu mwingine kwa malengo ya kuiboresha idara hiyo.
Amesema kuwa ikiwa ni miongoni mwa Mkoa unaotegemewa kwa uzalishaji wa chakula nchini haipendezi kwa idara hiyo kutokuwa na mpango sahihi wa maandalizi ya kilimo tangu kumalizika kwa msimu wa kilimo wa 2016/2017 hadi kuingia msimu wa kilimo wa 2017/2018 na kuiagiza idara hiyo kuwa karibu na waagizaji wakubwa wa mbolea kila ukikaribia msimu wa matayarisho ya mashamba kwa wakulima ili kujua kiasi cha mbolea kinachohitajika.
Ameyasema hayo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake fupi ya kutembelea maghala ya wafanyabiashara wakubwa wa mbolea ya mjini sumbawanga ili kujionea changamoto na mafanikio yaliyofikiwa baada ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa Mkoa wa Rukwa unapata mbolea ya kutosha ili wakulima waweze kufikisha lengo la uzalishaji wa chakula katika Mkoa.
Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa