Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemtaka Mkurugenzi wa Halmauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha anahamishia ofisi zake karibu na wananchi ambao wanishi katika mipaka ya halmashauri yake na sio kubaki mjini.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo mji utatanuka na maendeleo yatapatikana na pia kupunguza gharama za kuwahudumia wananchi pindi majanga yanapotokea kwani kuwa nao karibu kutasababisha kutotumia pesa nyingi kuwafuata na wao kupata urahisi wa kufika katika ofisi hizo.
“Rai yangu mkurugenzi mtafute mahala kwingine kwa kujenga ofisi za halmashauri ya wilaya, mahala pengine ambapo ni ndani ya halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na sio ndani ya manispaa, ofisi hii inapaswa iwe nje ya eneo la manispaa, faida yake ni kupanua huduma kuliko kila kitu kufikiria manispaa,” Alisema
Ameyasema hayo alipokwenda kukagua jengo jipya la halmashauri hiyo ambalo lilianza kujengwa mwaka 2012 na kutegemewa kumalizika mwaka 2013 japokuwa bado kukamilika ambapo serikali ilitenga shilingi bilioni 2.3 lakini hadi kufikia katika hatua ya sasa, tayari shilingi bilioni 1.6 zimeshatumika kupitia fedha za Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo (CDG) ambapo kwa sasa imefutwa.
Awali akitoa taarifa ya jengo hilo Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli amesema kuwa halmashauri tayari imekwisha tuma andiko maalum na kupeleka wizara ya fedha na OR – TAMISEMI ili kuwezeshwa kumalizia jengo hilo litakalokuwa na ofisi 76 na kumbi 2.
“Hadi sasa tumeandika andiko maalum la jumla ya shilingi 716,933,989 ili kukamilisha mradi huu, tunategemea jengo hili likikamilika litakuwa na ofisi 76 na kumbi 2 ambazo zitakuwa zinatosheleza mahitaji ya ofisi za watumishi wote walio katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya,” Alibainisha.
Jengo hilo ambalo lipo karibu na jengo la Manispaa ya Sumbawanga halijatengewa fedha za kuliendeleza tangu mwaka wa fedha 2015/2016 hadi sasa.
Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo alimuagiza Mkurugenzi huyo kuunda timu ya kuhakikisha wanapambana na mifugo inayoharibu barabara kwani serikali inatumia mabilioni kuzitengeneza na kuzikarabati na hivyo si vyema uharibifu huo ukaendelea.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa