Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amelitaka Baraza jipya la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhakikisha wanaongeza kasi ya kusimamia makusanyo ya mapato ili halmashauri hiyo iweze kutekeleza miradi yake ya kimaendeleo na hatimae kuwaridhisha wananchi waliowachagua kuwawakilisha katika baraza hilo.
Mh. Wangabo ameonya kuwa endapo halmashauri itashindwa kukusanya mapato ipasavyo mamlaka husika inaweza kuifuta halmashauri hiyo na hivyo kusababisha madiwani hao kuvuliwa nyadhifa zao hali itakayopelekea kuwekwa utaratibu mwingine wa kuisimamia halmashauri hiyo.
“Ikifikia hatua hiyo, waheshimiwa Madiwani mtakuwa mmewakosea sana wananchi ambao waliwachagua Pamoja na vyama husika kuwaleta hapa kwenye baraza la madiwani, kwahiyo lichukulieni kwa uzito mkubwa sana suala la mapato, kila unapolala, ukiamka fikiria mapato.”
Hata hivyo alisema kuwa haijawahi kutokea ukusanyaji wa mapato katika halmshauri hiyo ukafikia asilimia 100 au kuvuka na kuongeza kuwa itakuwa ni jambo jema kuona baraza hili la madiwani litasimamia ukusanyaji wa mapato na kufikia asilimia 100 na zaidi ili kurahisisha utekelezaji wa huduma za kijamii kwa maendeleo ya wananchi.
Aidha, alilitaka baraza hilo kuwa makini na wakusanyaji mapato ambao hutumia fedha walizokusanya kabla ya kufikisha benki (Defaulters) jambo ambalo ni kinyume cha sheria na hivyo kuwasihi madiwani hao wapya kuwapiga vita wakusanyaji hao kwa maslahi ya wananchi.
Mh. Wangabo ameyasema hayo tarehe 15.12.2020 alipokaribishwa kutoa nasaha zake baada ya wajumbe wa barazala la Madiwani Halmashauri ya Wilaya Nkasi kumaliza kula viapo vyao na kumchagua Mwenyekiti wa baraza hilo Mh. Pancras Maliyatabu Pamoja na Makamu Mwenye wake Mh. Wenslaus Kapita waliopitishwa kwa asilimia 86 za kura zote za madiwani 38.
Wakati akitoa salamu zake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda kabla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa alisema kuwa mwaka wa fedha 2020/2021 umemaliza miezi sita lakini makusanyo ya mapato katika halmashauri hiyo hayajafikia asilimia 38 na kuonya kujitoa katika kusuluhisha sintofahamu za posho za madiwani baina ya Mkurugenzi wa halmshauri hiyo na madiwani.
“Ikafika mahala madiwani wakaanza kukosa posho zao wakakopwa, kwahiyo kabla ya kikao cha baraza la madiwani hakijaanza ninaitwa Mkuu wa Wilaya kuanza kuzungumza na madiwani kwakuwa wengi ni Rafiki zangu niwasihi waende kwenye kikao kwahiyo wanakubali kwa heshima ya Mkuu wa Wilaya wanakubali kukopwa, kwahiyo baraza hili jipya linapoanza mhashimiwa Mwenyekiti na Makamu mimi suala la kuwa msuluhishi tena ninajiondoa,” Alisema
Pia alisisiza kuwa endapo madiwani hao watashindwa kuwasimamia watendaji wa serikali kuweza kukusanaya, kutumia kwa nidhamu na kudhibiti mianya ya matumizi mabovu ya fedha kitakachofuata ni wao kukosa haki zao na udiwani kukosa manufaa kwao na kwa wananchi wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Mh. Pancras Maliyatabu alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watayatumia vyema mamlaka waliyopewa juu ya kuwasimamia wataalamu hao wa halmashauri na kuwasihi wataaalamu hao kutowadharau madiwani huku akiwata madiwani hao kuweka mbele maslahi ya wananchi na kuwa mstri wa mbele kudhibiti upotevu wa mapato.
“Waheshimiwa madiwani tumepewa mamlaka kubwa sana, hivyo tukawatendee wananchi haki, kuna baadhi ya madiwani wanaacha mizigo inatoroshwa lakini wanakuja huku bila ya fedha wakijua watendaji wao hawajakusanya, wanakuja kuchukua posho huku, unakujaje kuchukua posho unaacha mizigo inatoroshwa? Kama sisi tumepewa dhamana ya kuisimamia halmashauri cha kwanza ni makusanyo,” Alisisitiza.
Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ilikusanya asilimia 90 na Mwaka 2018/2019 ilikusanya asilimia 94 na mwaka 2019/2020 Halmashauri hiyo ilikusanya asilimia 74 ya mapato ya ambayo ni Shilingi bilioni 1.9 kati ya Shilingi Bilioni 2.4 ya bajeti.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa