Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepiga marufuku mwalo wa mwambao wa Kijiji cha Kirando kutumika kama bandari baada ya kufika katika mwalo huo na kukuta lori likiwa linapakua mizigo kwa lengo la kusafisirisha mizigo kwenda kwenye visiwa vya ziwa Tanganyika.
Amesema kuwa wananchi wasipotoshe malengo ya mwalo huo ambayo ni kwaajili ya kuuza na kununua samaki wavuliwao kwenye ziwa Tanganyika, “Lengo la Mwalo huu ni kuuzia samaki na dagaa lakini naona mizigo hii, imegeuzwa kuwa bandari, narudia aliyoyasema Mh. Mbunge (Ali Kessy) irudishwe kwenye hali yake ile ile,” Alisisitiza
Mh. Wangabo aliongeza kuwa kama sehemu iliyokuwa ikitumika kama bandari hapako vizuri basi waone namna ya kupaboresha ili sehemu hiyo ilirudi kama ilivyokuwa na sio kuikimbia na kuiacha kama ilivyo na kusisitiza kuwa kukimbia tatizo sio suluhisho bali kupambana na changamoto zilizopo.
Awali kabla ya Kukaribishwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Ali Kessy alikemea kitendo cha wananchi hao wa Kirando kutumia mwalo huo kama bandari jambo ambalo ni kinyume na sheria na kuwasisitiza kuacha tabia hiyo mara moja.
“Nawaomba ndugu zangu kuanzia sasa hii sehemu isitumike kama bandari, hii sio bandari na haipo chini ya TPA, bandari ni ile ya zamani na iendelee kutumika ile ile na hapa tuwaachie wavuvi,” Mh. Kessy alimalizia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda aliwasisitiza wanaotumia vyombo vya ziwani kwa usafiri kuzingatia kuvaa maboya na kuonya kutozidisha mizigo na kuwa na abiria wengi kueleza kuwa watumiaji wa vyombo hivyo ndio wawe wa kwanza kutoa taarifa endapo wataona taratibu hizo zinakiukwa kwakuwa wasafirishaji hao huangalia faida kuliko usalama wa maisha ya abiria.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa