Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Nkomolo, kilichopo Namanyere Wilayani Nkasi pamoja na changamoto kadhaa zilizokuwa zikikabili maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Ametoa kauli hiyo alipofanya ziara katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya upanuzi wa majengo matano katika kituo hicho ikiwa ni miongoni mwa fedha za serikali zilizotolewa ili kuimarisha vituo vya afya nchini.
“Ujenzi huu ulianza mwezi Oktoba, 2017 na kutakiwa kuisha baada ya miezi mitatu lakini sasa ni mwezi wa nne lakini hiyo ni kutokana na changamoto ya ukubwa wa majengo haya ambayo yamesababisha kuchelewa kwa ujenzi huu, lakini mpaka sasa tumeridhika ujenzi unaenda vizuri, sasa rai yangu ni kwamba ujenzi huu ukamilike mwisho wa mwezi huu,” Alisema.
Mh. Wangabo alitumia nafasi hiyo kupongeza ujenzi huo kwa kuwashirikisha kina mama tangu mwanzo wa uchimbaji wa msingi hadi kumalizika kwa ujenzi huo na kuongeza kuwa ubora wa majengo huo unashinda ule unaojengwa na makandarasi ambao hutumia fehda nyingi kwa ubora usio wa uhakika.
Nae mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa ujenzi huo utaisha kwa wakati aliotoa maelekezo na kwamba hadi kufikia tarehe 2/3/2018 ujenzi huo pamoja na usafi wa mazingira utakuwa umekamilika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa