Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameshiriki katika ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Kalmabo pamoja na kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo na miradi mingine inayotekelezwa kwenye eneo hilo.
Ameshiriki katika Ujenzi huo baada ya kuvutiwa na ushiriki wa kina mama waliokuwa wakibeba ndoo za zege ili kundaa vitako vya mashimo ya nguzo 156 zitakazoshikilia jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Wilaya ya Kalambo jengo linalotarajiwa kuisha tarehe 26/6/2019 huku likigharimu shilingi Bilioni 4.1.
Eneo hilo lililotengwa rasmi kwaajili ya majengo ya kiserikali lina miradi mitatu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.99 ikijumuisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Nyumba yake pamoja na nyumba ya Tatibu Tawala wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na nyumba mbili za viongozi waandamizi wa Wilaya ya kalambo.
Katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa na mazingira mazuri Mh. Wangabo amewasisitiza wakandarasi na serikali ya Wilaya kuhakikisha wanapendezesha eneo hilo kwa kupanda miti ambayo ina kimo cha kuonekana ili miradi hiyo itakapokamilika na miti iwe ya kutoa kivuli.
Mbali na majengo hayo eneo hilo pia limejengwa nyumba sita za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo pamoja na ujenzi wa chuo cha ufundi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa