Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa Kata ya Paramawe yenye vijiji vitatu vya Lyazumbi, Paramawe ‘A’ na ‘B’ kuchangia shule moja ya msingi huku shule hiyo ikiwa na upungufu wa madarasa ya kuwahifadhi wananfunzi 1400 wa shule hiyo iliyopo wilayani Nkasi.
Amesema kuwa umefika wakati wa kila Kijiji katika kata hiyo kuhakikisha wanaanza ujenzi wa shule shikizi ili kuweza kuisaidia mzigo wa wananfunzi uliopo katika shule hiyo mama iliyopo katika Kijiji cha Paramawe ‘A’ na hatimae shule hizo shikizi zitakazoanzishwa katika vijiji hivyo ziendelezwe na kusajiliwa na kuwa shule kamili.
Ameyasema hayo wakati alipoitembelea kata hiyo ili kujionea maendeleo ya elimu ya shule ya msingi ambapo Kijiji cha Lyazumbi tayari kimeshajenga madara matatu yaliyokamilika pamoja na vyoo na ofisi ya walimu huku Kijiji cha paramawe ‘B’ kikikosa shule hiyo shikizi na hatimae kuwapeleka Watoto wa katika shule ya msingi Paramawe ‘A’.
“Muanze kujipanga sasa hivi, Mkurugenzi tuma watu waje wakae huku waone namna gani ya kuwasaidia hivi vijiji vitatu namna gani ya kuondokana na changamoto hii ya msongamano ya Watoto kwa kuhakikisha kwamba kila Kijiji kinakuwa na shule yake ya msingi na kwa kuanzia wawe na shule shikizi, weka mkazo mkubwa kumaliza ile shule ya msingi Lyazumbi na isajiliwe na hawa paramawe ‘B’ watafute eneo la kujengea shule hiyo,” Alisema
Aidha, katika kubainisha vigezo vya shule ya msingi kukamilika na kuweza kusajiliwa, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangula alivitaja vigezo vinne vinavyopelekea shule ya msingi kusajiliwa na kufafanua kuwa vigezo hivyo vimewekwa baada ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kubaini kuwa shule nyingi zikianzishwa kama shikizi na kusajiliwa huwa haziendelezwi na wananchi na hivyo kuupa mzigo serikali.
“Sasa hivi ili shule ya msingi isajiliwe lazima iwe na vitu vya msingi vinne, cha kwanza vyumba visipungue saba kwa maana ya darasa la kwanza mpaka la saba na cha pili kuwe na walau nyumba moja ya mwalimu kwasababu mwalimu mkuu lazima akae shuleni, lakini cha tatu lazima kuwe na vyoo vya makundi matatu vyoo vya wanafunzi wavulana na wasichana na vyoo vya walimu na cha mwisho ni viwanja vya michezo na hasa mpira wa miguu na “netball””, Alisema.
Shule Shikizi ya Kijiji cha Lyazumbi ina wanafunzi 375 wa darasa la kwanza hadi la tatu hali iliyomelekea Mtendaji wa Kijiji hicho Elizabeth Alex kuomba msaada wa nguvu za wananchi, serikali pamoja na wadau wa elimu nchini kusaidia ujenzi wa kumalizia shule hiyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa