Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu kikundi cha kinamama wanaojishughulisha na kazi za ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alipotemnbelea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya Nkomolo wilayani humo.
Amesema kuwa serikali itaendelea kutoa ajira kwa vikundi mbalimnbali kwa makundi yote ya wananwake na vijana wanaojishughulisha na ujenzi kutokana na kuwa na miradi mingi inayohitaji ujuzi wao na kuwaasa wanawake na vijana waige mfano huo ili waweze kujiwezesha kuliko kukaa vijiweni na kuendelea kuilaumu serikali.
“Nimependezwa na ujasiri wa hawa kina mama amabo sikutegemea kuwaona hapa, kwa namna wanavyofanya kazi nimefarijika sana, itabidi na wanawake wengine wanaokaa majumbani waige mfano wao kuliko kukaa tu na kusubiri kuletewa,” Alibainisha.
Ujenzi huo unaofanywa kwa mradi wa kuboresha vituo vya afya 172 nchini kwa fedha zilizotolewa na Wizara ya OR – TAMISEMI zilizochangwa na wadau wa maendeleo duniani wakiwemo benki ya dunia na wengineo.
Kwa upande wake mmoja wa wanawake hao Salome Sululu amethibitisha kuwa wamekuwa wakifaidika kwa kibarua hicho walichokipata na fedha wanazopatiwa kuwa zinawasaidia kujikimu katika familia na kuwawezesha kupata mitaji ya kujiendeleza kwenye kilimo na kusifu utaratibu wa serikali wa kuajiri vibarua wa maeneo husika bila ubaguzi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa