Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu juhudi za ujenzi wa jengo la huduma ya uzazi unaoendelea katika kituo cha afya cha Mazwi kilichopewa Shilingi Milioni 500 za Upanuzi na uboreshaji wa huduma za afya na Wizara ya OR – TAMISEMI.
Ameusifu utaratibu uliotumika katika ujenzi huo kwa kujumuisha maeneo matano muhimu katika jengo moja hali iliyopelekea kupunguza eneo la matumizi tofauti na wengine ambao wangeweka kila jengo na eneo lake kiasi cha kushindwa kutimiza mradi huo kwa wakati.
“RMO, Halmashauri, Mkurugenzi na maafisa wako wa Ujenzi mnafanya kazi nzuri, jengo lile mahali pengine pangekuwa namajengo kama matatu au manne lakini ninyi mmekuwa wabunifu kulingana na mazingira yenu, mkaunganisha,” Alisema
Akitoa maelezo kabla ya ukaguzi wa jengo hilo Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu amesema kuwa ujenzi umegawanyika katika majengo mawili ambapo jengo kubwa lina Wodi ya Uzazi, huduma ya kujifungulia na huduma ya upasuaji na jengo la pili lina Maabara na sehemu ya kuchomea taka na kuahidi kuwa hadi kufikia tarehe 20, Februari, 2018 ujenzi huo utakuwa umekamilika na kutumia kiasi cha shilingi Milioni 400.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa