Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesikitishwa na kitendo cha wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga kutohudhuria katika kikao muhimu cha mpango mkakati wa kuhakikisha mkoa wa Rukwa unaepukana na udumavu.
Amesema kuwa suala la udumavu katika mkoa ni jambo la kupewa kipaumbele kutokana na mkoa huo kuwa kinara katika udumavu kwa asilimia 56 huku kitaifa ikiwa ni aslimia 34 na kuongeza kuwa kitendo cha wakurugenzi hao kupuuzia jambo hilo kwa kutokuhudhuria wanaonesha namna ambayo wanarudisha nyuma juhudi za mkoa katika kuhakikisha wanapunguza udumavu mkoani humo.
“Vikao hatupo, mipango mingi, utendaji sifuri, mimi sio mtu wa kuzungumza sana, mi nataka kuona vitu vikienda, lakini kwa mwendo huu ambao ninauona hapa napoteza nguvu nyingi sana kwa matokeo sifuri, tangu jana nilikuwa napigana kuomba takwimu sijapewa labda watazisoma hapa kwamba mmekusanya kiasi gani dhidi ya kile ambacho kilipangwa mwaka jana na sasa tunaendelea kupanga hicho hicho ambacho tulikipanga huko nyuma, vikao hatupo mnatuma tu watu, sasa naona mkwamo kabla ya hata kupanga.” Alisisitiza
Alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akifungua kikao mpango wa lishe wa mkoa kilichowajumuisha wajumbe wa kamati ya lishe wa Mkoa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo katika ngazi ya halmashauri ya Weilaya ya Sumbawanga na halmashauri ya manispaa ya sumbawanga.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 kila halmashauri ilitakiwa kutenga shilingi 1000/= kwa watoto chini ya miaka mitano ambao wapo zaidi ya 240,000 katika mkoa na hivyo kutakiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 240 lakini hakuna hata halmashauri moja iliyoweza kufikia lengo la makusanyo hayo na kuzifikisha fedha hizo kwa wahusika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa