Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatakaka wakulima wa Kijiji cha Sakalilo kilichopo kata ya Ilemba, Wilayani Sumbawanga kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao yao ili kuuza kwa bei nzuri nahatimae kusafirisha katika maeneo mbalimbali ya nchi kwani kufanya hivyo kutawapelekea kujitangaza na hatimae kuongeza wigo wa soko.
Ameyasema hayo alipotembelea ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao katika Kijiji cha Sakalilo chenye wakati wapatao 1192, Mradi huo unafadhiliwa na AGRA kupitia mradi wa TIJA na unatekelezwa na sekta binafsi ambao ni shirika la MIIC, ambapo ghala hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 450 na utagharimu shilingi milioni 155 na kutegemewa kuhudumia wakulima wapatao 500.
“Mfikirie kuyaongezea thamani mazao haya kuna watu wanatokea mikoa ya jirani wanakuja kuchukua mpunga hapa wanakwenda nao kwao halafu wanaongezea thamani na kuandika wa kwao wakati unatoka Sakalilo, hivyo ghala hili lisiwe tu kwaajili ya kuhifadhia mazao kusubiri bei ipande lakini pia mfikirie kuweka mashine kwaajili ya kuyaongezea thamani mazao hayo,” Alisema.
Kwa upande wake Afisa biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Shabani Bahari alisema kuwa fedha za ujenzi wa ghala hilo zimepatikana kutoka vyanzo mbalimbali na unategemewa kumalizika ndani yam waka mmoja tangu kuanza ujenzi wake.
“Ujenzi huu ulianza tarehe 13.3.2018 na utamalizika tarehe 15.4.2019 na kugharimu shilingi milioni 155 ambapo mpaka sasa milioni 15 ni nguvu ya wananchi, shilingi 700,000/= zimetolewa na Sakalilo AMCOS kwaajili ya kiwanja na Shilingi milioni 80.5 zimetolewa na wafadhili,” Alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sakalilo AMCOS Osward Sinkala amesema kuwa ghala hilo litakuwa mkombozi kwa wakulima wa kata nzima ya Ilemba na kuongeza kuwa mipango iliyopo ni kukusanya mazao kuanzia mwezi wa 4, na kufafanua kuwa tayari wameshaongea na benki ya NMB ili kuweza kuwawezesha wakulima watakaohifadhi mazao yao kwenye ghala hilo kupata mkopo na pindi bei itakapopanda waweze kuuza na kurudisha mkopo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa