Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa Mkoa wa Rukwa na watanzania kwa ujumla kujenga mazoea ya kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo kwenye maeneo yao ili kujihakikishia soko la ndani na hatimae kuvuka mipaka ya nchi.
Ameyasema hayo baada ya kutembelea Kiwanda cha Unga Energy Sembe na Kiwanda cha maji Dew Drop vinachomilikiwa na Azizi Mohamed Sudi, Mbasira Fodd Industries na Kiwanda cha maziwa OTC Kizwite kinachomilikiwa na kikundi cha wafugaji vyote vikipatikana katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa vinavyozalisha bidhaa zinazouzwa ndani ya Mkoa, nje ya Mkoa na kuvuka mipaka ya nchi.
Amesema kuwa Kazi ya Serikali kutoa mazingira bora na wezeshi ili wawekezaji wawe na fursa nzuri za kuwekeza na kuongeza kuwa serikali haitakubali kuona viwanda vikifa kwa mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wa serikali na kuwahakikishia wamiliki wa viwanda hao kuwa serikali haiwezi kuendelea kuhamasisha viwanda bila ya kutatua changamoto mbalimbali zinazokumba viwanda vilivyopo.
“Tujivunie viwanda vyetu vya hapa, hasa vile vinavyozalishwa na wazawa wenyewe ambavyo vinatoa ajira kwa wananchi wa Mkoa huu, changamoto zipo kama masuala ya kimazingira, malighafi na umeme, kama serikali tutayachukua ili kuhakikisha wawekezaji wanafanya kazi katika mazingira bora kabisa, kazi ya serikali kuweka mazingira wezeshi ili wenzetu waweke viwanda ili tuweze kufikia uchumi wa kati wa Viwanda kufikia 2025,” Alisema.
Na kushauri kuwa viwanda hivyo havinabudi kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ili kuweza kupata masoko ya uhakika.
Kwa upande wake Mmiliki wa Kiwanda cha Unga Energy Sembe na Dew Drop, Aziz Mohamed Sudi amesema kuwa kiwanda cha sembe kimesimama uzalishaji wake tangu Mei, 2017 baada ya kukosa soko la ndani ya nchi na kutegemewa kuanza tena mwaka 2018 baada ya kupata maombi kutoka nchi ya Kongo.
“Wawekezaji katika mikoa ya pembezoni tumekuwa mbali na masoko makubwa, gharama za uzalishaji, umeme na kupeleka bidhaa hizo kwenye masoko makubwa zimekuwa kubwa pamoja na pamoja na utititiri wa kodi, hivyo tunaiomba serikali iruhusu kuuza bidhaa za kiloimo zilizoongezwa thamani na tunakubalina na hatua za kudhibiti chakula kwa kuuza nafaka,” Azizi Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa