Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesisitiza Uwajibikaji, na kujituma kwa watumishi wote wa serikali mkoani humo ili kuweza kupeleka mbele gurudumu la maendeleo na kuwatumikia wananchi ambao wapo ili waweze kuhudumiwa na watumishi.
Amesema kuwa bila ya uadilifu katika matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali katika halmashauri hakutakuwa na maendeleo lengwa jambo litakaoiingizia serikali hasara na kurudi nyuma kimaendeleo.
Ameyasisitiza hayo alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika ziara yake ya siku mbili iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya halmashauri pamoja na kujitambulisha kwa watumishi na makundi mbalimbali ya wananchi katika wilaya.
“Jambo ninalosisitiza la kwanza ni uwajibikaji, kila mtumishi wa serikali anatakiwa kuwajibika kufanya kazi kwa bidii na kujituma, kwani serikali hutoa pesa nyingi za miradi ya maendeleo hivyo tusipokuwa waadilifu na kufanya kazi kwa bidi rasilimali zetu tutazipoteza, tunataka thamani ya fedha ionekane huko kwenye utekelezaji wa miradi hiyo,” Alisisitiza.
Pamoja na hayo RC Wangabo amewataka watumishi hao kuwa wanyeyekevu wanapokuwa wanawahudumia wananchi na kutotumia vyeo vyao kuwanyanyasa wananchi hao kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakiogopa kuingia kwenye ofisi za kiserikali ili kutatuliwa changamoto na matatizo yanayowakumba kutoka katika maeneo yao.
Amesema kwa kufanya hivyo kutaipa sifa serikali na pia kujiwekea akiba ya uaminifu kwa wananchi wanaopewa huduma hiyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa