Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa viongozi, watendaji, na wananchi wa mkoa kuhimizana kutunza mazingira kwaajili ya manufaa ya kupata mvua za uhakika, ili kuweza kufuga nyuki kwani kutofanya hivyo fursa zote zitapotea.
Pia ameongeza kuwa ongezeko la kilimo cha alizeti ni fursa kwa nyuki kutengeneza asali na chakula chao na utunzaji wa mazingira hupelekea kuongezeka kwa mvua hali inayopelekea uwepo wa mimea mbalimbali ambayo nyuki hutengeneza asali.
“Napenda kutoa msisitizo kuwa kuna muunganiko wa karibu baina ya utunzaji wa mazingira, ufugaji wa nyuki na uendelezaji kilimo na kuongezeka kwa kipato, hivyo nawaasa kuanzisha vikundi ambavyo vitakuwa na sifa za kupata mikopo kwaajili ya kuendeleza ufugaji bora wa nyuki,” Mh. Wangabo Alisisitiza.
Ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa mizinga ya nyuki katika shamba la SAAFI LTD lililopo katika Kijiji cha Nkundi, Wilayani Nkasi, ambapo mapaka sasa Mkoa wa Rukwa una jumla ya wafugaji nyuki wakubwa 12 wenye mizinga isiyopungua 100, na wafugaji wadogo wapo 58,184.
Gharama za kutengeneza mzinga mmoja wa nyuki ni wastani wa Shilingi 40,000/= hadi 50,000/= na mzinga mmoja unatoa lita 20 za asali ambayo kwa bei ya soko ni shilingi 8,000/= kwa lita na hivyo kufanya lita 20 kuwa ni shilingi 160,000/=.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa