Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kutangaza maeneo mbalimbali ya uwekezaji yaliyopo mkoani Rukwa ili kuunga mkono kauli mbiu ya wiki ya mahakama Tanzania.
Pia amewaasa wananchi kutumia fursa zilizopo za biashara na uwekezaji katika kujiendeleza kimaisha na kuinua hali zao, na kuongeza kuwa Maendeleo ya kimaisha katika biashara yatatoa nafasi ya maendeleo katika nyanja nyingine hususani huduma za Jamii.
“Ni Imani yangu kuwa Halmashauri pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ambazo kwa njia moja ama nyingine zinahusika katika kukuza Biashara na Uwekezaji zitaendelea kutoa elimu ya biashara, kutangaza maeneo ya uwekezaji yaliyopo katika Mkoa wetu na kuhakikisha biashara zinafanyika katika mazingira rafiki ili kukuza uchumi na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.” Alisema.
Ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mahakama yaliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini Sumbawanga wakati akitoa salamu za Mkoa.
Aidha ameutaka Muhimili huo wa Mahakama kujiepusha na Rushwa ili kutenda haki kwa wananchi bila ya kujali vipato vyao na hivyo kumsaidia yeye kupunguza msururu wa watu wanaokwenda ofini kwake kutaka kuingilia kati vitendo vinavyofanywa na watendaji wa mahakama jambo ambalo linachafua muhimili wa mahakama.
Kauli mbiu ya mwaka 2020 ya wiki ya mahakama “uwekezaji na biashara; wajibu wa mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji”.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa