Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha anampatia taarifa inayoonyesha mchanganuo wa matumizi ya fedha zilizotumika kupanua kituo cha Afya cha Milepa ili waweze kuwaeleza wananchi namna fedha hizo zilivyotumika na kiasi kilichookolewa kutokana na songambele walioifanya wakati wa uchimbaji wa misingi wa kituo hicho.
Kituo hicho ambacho kilipewa shilingi milioni 400 na serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwaajili ya kujenga majengo matano ikiwemo, chumba cha upasuaji, Mochwari, maaabara, nyumba ya watumishi pamoja na wodi ya kina mama, hadi sasa imebakisha kumalizia jengo la watumishi ili kumaliza upanuzi huo.
“Huu mpango wa kusomeana taarifa kiujumla jumla mimi siukubali, kwamba ujenzi mpaka sasa umeshatumia milioni 340 bila ya mchanganuo mimi sielewi, kwahiyo ninataka ripoti ya kina hii sijaikubali, mtuandikie mtuandalie vizuri sana halafu muiwakilishe katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama, tutawapangia siku ili mtuambie ile mochwari mlitumia shilingi ngapi mpaka kufika pale na majengo mengine,” Alibainisha.
Aliyasema hayo alipotembelea kituo hicho cha afya ili kujionea maendeleo ya upanuzi wa kituo hicho na kuelekeza ujenzi huo umalizike haraka ili wananchi waanze kukitumia, kwani wamekisuburi kwa muda mrefu na muda wake uliopangiwa kumalizika umeshapita tena kwa miezi sita, kwani kituo hicho kilitakiwa kuisha mwezi Mei mwaka huu.
Wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Nyangi Msemakweli alisema kuwa miongoni mwa changamoto kubwa wanayoipata katika kukamilisha ujenzi huo ni pamoja na kupata mafunzi wenye utaalamu ambao wengi wao hawapo mkoani Rukwa na matokeo yake kuzorotesha kasi ya ujenzi.
“Majengo hayo yote yako katika hatua za mwisho kama ulivyokuwa umeona katika ukaguzi yakiwa yamebakiza vipengele vidogo vidogo vingi vikiwa ni usafi wa mwisho isipokuwa jengo la upasuaji ambalo linahitaji fundi wa sakafu maalum kwenye chumba cha upasuaji, ambapo kuna changamoto ya kumpata fundi wa kukipiga sakafu kwenye chumba hicho, lakini tumefanya jitihada na kubaini kuwa fundi mwenye uwezo yupo mkoa wa Katavi na atapatikana.” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa