Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya kumpatia taarifa juu ya miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.2 iliyokataliwa na Mwenge wa uhuru katika halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa awali mwenge huo ulitarajiwa kuzindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi yenye thamani ya shilingi 20,499,194,896 vikiwemo vikundi 48 lakini kutokana na kasoro zilizojitokeza Mwenge huo uliweza kuweka mawe ya msingi, kukagua na kuzindua miradi yenye thamani ya shilingi 18,226,464,641.
“Napenda nitoe maelekezo kwa waheshimiwa wakuu wa wilaya kunipa taarifa kwanini miradi yao haikuzinduliwa, maelezo hayo nitayapata ndani ya siku tatu kuanzia leo hii, aidha nipende kuwashukuru sana wakimbiza Mwenge ambao kwa maelekezo yao na ushauri wao niseme vyote tutavizingatia,” Alisema.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Charles Kabeho alisifu mapokezi mazuri aliyoyakuta katika miradi yote aliyoitembelea mkoani Rukwa na kuongeza kuwa kama ingelikuwa ni mapenzi yake basi angependa kuendelea kuwepo Rukwa ila kutokana na majukumu ya kitaifa hana budi kwenda Mkoa wa Songwe.
Miongoni mwa miradi iliyokataliwa ni mradi wa maji wa Laela katika halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pamoja na nyumba za watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa