Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza mkurugenzi wa halmasshauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha anampatia taarifa ya kila wiki juu ya maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Kanyezi, kilichopo kata ya Kanyezi wilayani Kalambo.
Maesema kuwa tangu kuanza kwa miradi ya upanuzi na ujenzi wa vituo vya afya katika halmashauri hiyo kumekuwa na ubabaishaji hasa wa kuchelewa kununua vifaa vya ujenzi pamoja na malipo kwa mafundi ambapo ujenzi huo unatumia mfumo wa “Force Account” kutekeleza kazi hiyo.
“Sasa wewe afisa mipango, Mkurugenzi, kuanzia sasa hivi nataka muwe mnanipa taarifa “on weekly basis” (za kila wiki) kwamba nini kinachoendelea katika ujenzi huu, nisingependa tabia hii ya kusua sua iendelee, muiache mara moja, mnaumiza hawa wajenzi, halafu hamuwezi kuwalipa fidia, ingekuwa hawatimizi wajibu wao ingekuwa kitu kingine, kama ilivyotokea kule Kijiji cha Legeza mwendo fundi akakimbia ni kwasababu ya namna hii ubabaishaji wa malipo, mjipange,” Alisisitiza.
Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kimepandishwa hadhi kutoka kuwa zahanati ya kijiji cha Kanyezi na kukuta zimebaki siku 15 kutakiwa kukabidhi majengo hayo lakini bado wapo katika hatua ya linta.
Kwa upande wake Afisa Mipango wa halmashauri hiyo Bw. Erick Kayombo aliahidi kuwa pamoja na kucheleweshewa kupata fedha lakini halmashauri tayari imeshaagiza vifaa vyote vinavyotakiwa kwaajili ya kumalizia ujenzi.
Kauli hiyo ya Mh. Wangabo ilikuja baada ya mmoja wa mafundi wadogo bw. Hamisi Pesambili kumlalamikia Mkuu wa Mkoa juu ya kucheleweshewa vifaa kwaajili ya kuendelea na ujenzi hali inayowafanya waishi kwa taabu huku wakiwa wameacha familia zao mjini sumbawanga na kwa siku kulipwa shilingi 10,000 fedha ambayo hawaridhiki nayo.
Katika kulirekebisha hilo, Mh. Wangabo alimuagiza mhandisi wa Halmashauri ambaye pia ni msimamizi wa jengo hilo kuhakikisha kuwa wanasimamia malipo ya mafundi wadogo kutoka kwa mafundi wao na sio kuishia kuwalipa mafundi huku hawajui kama vibarua hao wanalipwa kama walivyokubaliana na mafundi wao na kuongeza kuwa kutolipwa vizuri kwa vibarua kunaweza kupelekea majengo kutokuwa na ubora unaotarajiwa.
Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kujenga vituo vitatu vya afya katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na kutumia zaidi ya shilingi bilioni moja kwaajili ya ujenzi na utanuzi huo huku ikielekeza shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa