Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya kalambo kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa kituo cha afya cha mwimbi, kituo kilichoanza kujengwa tarehe 1/8/2017 na kufikia hatua ya kupauliwa.
Mkandarasi wa ujenzi huo mwakilishi wa SUMA JKT amesema kuwa kinachokwamisha kuendelea kwa ujenzi huo ni fedha ambapo wameomba kuidhinishiwa shilingi milioni 120 ili kuendelea na hadi Mkuu wa Mkoa anawasili kukagua maendeleo ya ujenzi huo fedha hizo hazijafika huku siku 14 zikiwa zimekatika bila ya mafanikio.
“Baada ya mwezi mmoja nitakuja hapa mnikabidhi wenye jengo likiwa limekamilika, hakuna sababu ya kuchelewesha kama fedha ipo, mkandarasi yupo, kwanini ujenzi umekwama, Mkurugenzi ndani ya siku mbili fedha hiyo iwe imetoka ili washambulie hili jengo liweze kuisha, vitu vichache sana vimebaki hapa” Alisema.
Na kuongeza kuwa uzembe huo ndio unaosababisha usumbufu wa huduma za afya kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo hasa kina mama na watoto chini ya miaka mitano jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais mpendwa Dk. John Pombe Magufuli.
Awali akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi huo Mwakilishi wa SUMA JKT amesema kuwa tangu kuanza kwa ujenzi huo wametumia shilingi milioni 50 kati ya shilingi milioni 355 ambazo zinatakiwa kutumia hadi kumaliza mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 400.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa