Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewashauri wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi na Kalambo kuchangamkia fursa ya kibiashara iliyojitokeza baada ya operesheni ya kukamata wavuvi haramu na wasafirishaji wa samaki wanaotumia magari ya abiria kuzuiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003.
Amesema kuwa sheria hiyo hairuhusu mabasi ya abiria kupakiza samaki wanaozidi kilo 20 ambao katika hali ya kawaida ni samaki wa kitoweo nyumbani tofauti na hapo ni samaki wa biashra ambao mwananchi anatakiwa kulipia ushuru na kuongeza kuwa bidhaa hizo zinakuwa na magari yake maalum kwaajili ya kazi hiyo ambayo kwa sasa hayapo katika kusafirishia samaki kutoka mwambao hadi sumbawanga mjini.
“Kuna mazingira ambayo lazima sisi wenyewe tuanze kuyawekea utayari na watu wengine wachukulie kama fursa, kama unaambiwa samaki wasafirishwe kwa chombo fulani kilicho maalum, basi wafanyabiashara wengine chukueni hiyo ni fursa kwenu, nunueni hilo gari, sio kwamba wote ni wafanyabiashara wadogo hapa wapo wenye uwezo, lakini pia mnaweza kuungana mkakopa hilo gari na sisi tutawadhamini,” Alisisitiza.
Alitoa kauli hiyo baada ya wavuvi kumlalamikia Mkuu wa Mkoa kuhusu kuzuiwa kusafirisha samaki kwa kutumia magari ya abiria jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa