Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo ametoa ushauri kwa wadau wa michezo nchini kuona namna ya kuimarisha mbinu za kuibua vipaji vya wanamichezo kuanzia ngazi ya shule za msingi katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ili kuweza kuwa na vijana watakaoweza kubeba jina la Tanzania katika michezo.
Amesema kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliochelewa kulala ili kuangalia mechi baina Tanzania maarufu kama Taifa Starts na jirani zetu Kenya maarufu kama Harambee Strars ambapo hadi kumalizika kwa mchezo huo Harambee Stars iliibuka kidedea kwa kuilaza Taifa Stars mabao 3 kwa 2.
“Kuna ambao wamelala alfajiri na wengine wapo humu ambao wamelala leo, tunaomboleza kufungwa huku, tungeshinda jana tungekuwa na mwanga wa kusonga mbele, sasa ni kinyume na yalivyokuwa matarajio yetu lakini ndugu wana Rukwa tusikate tamaa, tuendelee kuiunga mkono timu yetu hii ya Taifa, Kufungwa ni kujifunza, tuendelee kujipanga vizuri hasa kwa vijana kuanzia UMISHAMTA huku mpaka UMISETA na kwenye “academy” hizi,” alieleza.
Aidha, alibainisha kasoro kadhaa zinazojitokeza katika ligi yetu ya Tanzania hasa kwa upande wa timu vinara zinazopata nafasi za kwenda kucheza makombe ya Kalbu Bingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho kuona namna ya kutoa fursa kwa wachezaji wa kitanzania ili wapate ujuzi wa kimataifa na sio kuwajenga wachezaji wa nje ambao wanakwenda kutumikia nchi zao.
“Hizi timu zetu za Yanga na Simba pamoja na Azama zinafanya vizuri kwasababu zina wachezaji wengi wa kigeni matokeo yake timu ya Taifa inapokwenda kwenye mashindano wachezaji wetu wanabaki wenyewe, angalieni Emanuel Okwi anavuma kule Uganda lakini tumemuwezesha sisi hapa Tanzania,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa