Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa wasanii mbalimbali nchinipamoja na timu za mpira wa miguu kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani ikiwemo kutembelea maporomoko yam to Kalambo, yaliyopo katika hifadhi ya mto Kalambo, Wilayani kalambo.
Amesema kuwa kwa muda mrefu maporomoko hayo yamesahauliwa na wananchi waliomo nchini hivyo ni wakati muafaka kuanza kuyatangaza maporomoko hayo ili yaweze kufahamika na wananchi wa ndani na wa nje na matokeo yake Mkoa utambulike na kuliingizia taifa mapato.
“Natoa wito kwa wasanii mbalimbali waje wachukue picha kwenye mandhari hii watangaze utalii wa nchi yetu na utalii katika Mkoa wetu wa Rukwa, Rukwa sasa hivi imefunguka kuna maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa ndege mkubwa kule Kisumba, uwanja huo ukishajengwa bila ya shaka eneo hili litakuwa linachanganya sana katika utalii na nchi yetu itaboreka katika uchumi, mara ya mwisho ilikuja timu ya Simba ikaishia Sumbawanga naziomba timu zote za ligi kuu kuja kuyaona maporomoko ya kalambo” Alisema
Kwa upande wake Kaimu meneja wa Wakala Huduma za Misitu (TFS) Wilayani Kalambo Chesco Lunyungu amesema kuwa wamejitahidi kufungua njia inayofika hadi chini ya maporomoko hayo jambo ambalo kwa upande wa Zambia hawawezi kufika chini maji yanapomwagika hivyo kwa kupitia mkandarasi Green Civil and Construction Ltd, tayari ngazi yenye urefu wa mita 217 imeshajengwa ili kuweka mazingira mazuri ya watalii kuweza kufika pale maji yanapoagukia ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 95.
Ameongeza kuwa ujenzi huo umegharimu Shilingi milioni 76 huku ujenzi huo ukiendelea ambapo hadi kukamilika kwake kunahitajika Shilingi Bilioni 1, tofauti na ngazi hizo pia kuna njia za kuchonga zenye urefu wa mita 500 za kumuwezesha mtalii kufika eneo la maji yanapomwagika pamoja na kuandaa maeneo mawili ya kupumzikia watalii “Campinga Site”
“Maporomoko haya yana urefu wa mita 235 na ni ya pili kwa ukubwa katika afrika na pia vivutio vilivyopo ni vya pili kwa uzuri katika bara la Afrika ambavyo ni pamoja na muda wote kuwa na upinde wa mvua “rainbow” pale maji yanapoanguakia ambao watalii wanavutiwa sana, pamoja na uoto wa asili unaopatikana chini ya maporomoko hayo.” Alisema.
Maporomoko hayo yanapatikana katika hifadhi ya mto Kalambo, yenye ukubwa wa hekta 534.9 mpakani mwa Tanzania na Zambia ambayo yapo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yenye urefu wa mita 235.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa