Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amevionya vikundi vya kidini vinavyoanzishwa baada ya kutokea migogoro kwenye makanisa na misikiti kufuata sheria katika kufanya shughuli zao za kiibada na sio kujianzisha kiholela.
Amesema kuwa kila mtanzania ana uhuru wa kuabudu akiwa mmoja lakini linapokuja suala la kikundi basi hakuna budi kikundi hicho kifuate taratibu za kujisajili ili kiweze kutambulika na vyombo vya serikali kwani vyombo vyote vya kidini vinatambulika kisheria na vimesajiliwa.
“Imani ya mtu mmoja mmoja mtu aabudu tu hata chini ya meza, popote tu, lakini unapokusanya watu, kwasababu tusipokuwa makini hawa wanaokusanya watu bila kujua wana katiba gani na miongozo ipi, kesho watachoma moto hawa waumini, si mnakumbuka yaliyotokea Uganda, halafu lawama itarudi kwa serikali, hatutaruhusu hilo, ” Alisisitiza.
Amesema kuwa vukundi vinavyojitenga huanzisha mikusanyiko yao katika nyumba za kawaida na hufanya kazi kama kanisa japokuwa hawajasajiliwa, hivyo kama serikali itavitafuta vikundi hivyo na kuhakikisha vinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu.
Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na uongozi wa kanisa la KKKT Tanzania walipomtembelea ofisini kwake.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa