Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim wangabo amesikitishwa na kitendo cha wafanyabiashara kutumia mbinu mbalimbali za kukwepa kulipa kodi serikalini jambo linalorudisha nyuma maendeleo, hivyo kutoa siku saba za kujirekebisha kabla ya Mamlaka ya mapato kuanza msako mkali na kuwatia nguvuni.
Amesema kuwa katika kipindi cha mitatu kuanzia Oktoba hadi Disemba, 2017 Mamlaka ya Mapato Rukwa imekusanya shilingi bilioni 2.2 kiasi ambacho hakiendani na uhalisia na kuongeza kuwa Mamlaka hiyo inaweza kufanya vizuri zaidi endapo itapambana na vipingamizi vilivyopo.
“Kuna vipingamizi kadhaa moja ni wafanyabiashara kutokuwa na EFD, pili, baadhi ya wafanyabiashara kutotoa risiti, kuna wenye EFD mbili, iliyosajiliwa na isiyosajiliwa, na wao hutumia isiyosajiliwa na wengine kuwa na vitabu viwili vya stakabadhi na kutumia kile chenye mapato madogo kupiga mahesabu ya serikali, yote hii ni mianya ya kukwepa kodi ya serikali,na wengine kuuza kwenye magari bila ya risiti,” Alisisitiza.
Pia amebainisha kuwa kuna wafanyabiashara 316 ambao wamelipia mashine za EFD lakini hadi leo hawajapewa mashine hizo na kusababisha kuvuja kwa mapato ya serikali, ameyasema hayo katika mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa.
Katika kubainisha changamoto za wafanyabiashara mkoani humo Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara ,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Rukwa Sadrick Malila amesema kuwa wafanayabiashara mkoani humo wamekuwa na wakati mgumu kutokana na utitiri wa kodi na kutokuwa na mahusiano mazuri na Mamlaka ya mapato Tanzania na kushauri kurudishwa kwa Jukwaa la walipa Kodi kwani lilikuwa na manufaa.
“Tulikuwa na jukwaa la walipa kodi, amabapo tulikuwa tunakaa na kujadili, lakini hili jukwaa limefutwa na kutoka pale imekuwa ubabe na wakati ule TRA walikuwa wanavuka malengo kuliko hali ilivyo hivi sasa,ambapo hawavuki malengo”Alisema
Tuhuma hizo zilikanushwa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato TRA Mkoani Rukwa Fredrick Nyariri nae kutoa takwimu zilizobainisha kuvuka kwa malengo kulingana na viwango walivyopangiwa.
“Si kweli kwamba hatuvuki malengo kwa mfano mwezi Novembea tulipangiwa Shilingi Milioni 801 tukapata Milioni 928 na Mwezi Disemba tulipangiwa kukusanya Shilingi Milioni 908 na tukapata Milioni 996, nasikitika kusema kwamba taarifa ya mwenyekiti TCCIA imejaa upotoshaji,” Alimalizia.
Na kuongeza kuwa Mamlaka ya Mapato imejipanga kuuza mashine za EFD na kuepukana na kuwa na wakala mmoja wa kusambaza mashine hizo ndani ya Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa