Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasihi wazee wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kutokaa kimya pindi wanapoona wataalamu wa halmashauri hiyo wanakwenda tofauti na uhalisia wa mambo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo.
Amesema kuwa kumekuwa na miradi mingi inayokwama kwasababu ya wataalamu hao kushindwa kujua historia za sehemu husika na matokeo yake serikali inapoteza pesa nyingi kufanya marekebisho ya miradi hiyo pale panapotokea hitilafu inayogharimu halmashauri na maisha ya wananchi wanaotegemea ukamilifu wa miradi hiyo.
Ametoa kauli hiyo alipofanya kikao na umoja wa wazee wa halmashauri ya Nkasi katika ziara yake ya siku mbili kwenye halmashauri hiyo yenye lengo la kutembelea miradi na kujitambulisha kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
“Mkiona mambo yanakwenda sivyo kwenye mradi mnajikusanya, Mwenyekiti na Katibu hapa mnakwenda kumuona mkurugenzi na kumshauri, hayo ndio maendeleo shirikishi na maendeleo shirikishi hayawabagui wazee, wazee nao wana neon lao katika maendeleo.” Alisisitiza.
Aidha aliwasisita kuendelea kudumisha maadili katika jamii ili kupunguza mimba kwa wananfunzi wa Wilaya ya Nkasi ambazo zinazoendelea kuzorotesha maendeleo ya wanafunzi wa kike na kuwaomba watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola pale inapotokea jambo hilo. Na kubainisha kuwa katika kipindi cha miezi 6 tangu kuanza kwa mwaka huu mimba 46 zimebainika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa