Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha mafundi na vibarua wa mradi wa ujenzi wa vihenge unaojengwa na serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kuwa makini na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona kwa kufuata maelekezo ya wataalamu afya wawapo katika eneo la kazi na wanaporudi kwenye familia zao.
Amesema kuwa afya ya kila mmoja ni muhimu kutokana na mchango wake katika kujenga nchi na hivyo kuwataka kuwa makini kwa kunawa kila mara hali iliyopelekea kumuagiza meneja wa mradi huo kwa niaba ya Wakala wa majengo nchini (TBA) Mhandisi mkazi Haruna Kalunga kuhakikisha eneo hilo la kazi kunakuwa vifaa vya kutosha vya kunawia maji na sabuni kwa kukanyaga kwaajili ya wafanyakazi na kuondoa ndoo zilizopo ambazo koki zake hazina usalama.
“Afya yako ni ya Msingi sana, na familia yako na sisi sote kwa ujumla wake, kwa maana wewe mtu mmoja ukiugua Corona utaweza kuusambaza kwa watu wengi sana, na wote hapa mnaweza mkafutika ndani ya wiki moja tu, sasa mtakuwa mmeiweka nchi mahali pabaya na mradi wenyewe utasuasua, kwahiyo mjihadhari na ugonjwa huu hatari wa Corona, lakini mchape kazi msiogope kuchapa kazi,” alisema.
Aidha, alitoa pongezi kwa mkandarasi wa mradi huo Unia araj kutoka nchini Poland kwa kusaidiana na mkandarasi mzawa Elerai kutoka Arusha pamoja na meneja wa mradi huo TBA pamoja na mafundi wa mradi huo kwa kufanya kazi ndani ya wakati mbali na hali ya hewa kutokuwa Rafiki kwa ujenzi huo na hivyo kuwataka kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi huo ifikapo tarehe 9.3.2020.
“Ningependa ratiba hiyo izingatiwe, tusirudi nyuma tuongeze kasi kwa kiwango ambacho mradi huu tunataka umalizike mapema, utakuwa na manufaa makubwa sana kwasababu uwezo wa kutunza nafaka zetu kimkoa utaongezeka kutoka tani 30,500 za sasa mpaka kufika tani 55,500 utakuwa ni uwezo mkubwa, kwahiyo hata wakulima wetu watahamasika kulima mahindi zaidi wakijua kwamba NFRA itaweza kuyanunua na kuyahifadhi kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi,” Alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa TBA Mhandisi Mkazi Haruna Kalunga alisema kuwa ujenzi huo utajumuisha majengo 13 ambapo ujenzi wa vihenge 6 vikubwa na vihenge 2 vidogo pamoja na miundombinu yake itachukua asilimia 70 ya mradi huku asilimia 30 ikibebwa na majengo saidizi.
“Kuna Jengo la utawala, kuna jengo la kupikia na kulia chakula, kuna jengo la kutunzia vifaa na dawa, kuna jengo la maabara kwaajili ya upimaji wa hizo sampuli ambazo zitakuwa zinaingia hapa, kuna vihenge 6 vikubwa na vihenge vidogo kwaajili ya usafi vyenye jumla ya tani 20,000 na pia tuna ghala la kuhifadhia mazao lenye uwezo wa kubeba tani 5,000,” alisema.
Kwa mkoa wa Rukwa mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani 6,019,399.00 wakati mkandarasi huyo akifanya kazi katika mioa mingine ya Manyara na Katavi ambapo jumla ya gharama yake ni $20,280,906.00 ambapo hadi sasa mkandarasi huyo ameshalipwa $ 10,175,714.22.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa