Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameyaomba mashirika binafsi kuona umuhimu wa kuwawezesha wafungwa wanaotoka magerezani kupitia mpango wa ‘parole’ ili wafungwa waweze kupata kianzio cha maisha wanaporudi uraiani kuendelea na maisha yao.
Amesema kuwa wafungwa wengi wanaotoka kwa mpango huo wanakuwa wametumikia kifungo cha zaidi ya miaka minne gerezani na watokapo huwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri na kuweza kuendelea kulitumikia taifa katika kukuza uchumi na kuacha kuwa tegemezi katika familia.
“Kumbuka kuwa wamekaa zaidi ya miaka minne hivyo wanapotoka kule wanakuwa na changamoto kubwa sana ya kuanza maisha ingawa wanakuwa na ujuzi wao, na wakati mwingine hata jamii inawanyanyapaa, kwahiyo Taasisi zisizo za kiserikali ni vyema zikaunga mkono mpanpo huu ili kuwawezesha kuwapatia kianzio cha maisha n ahata kukuza ujuzi walionao ili wajione ni sehemu ya jamii,” Alifafanua.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Parole Mkoa wa Rukwa ambayo hudumu kwa miaka mitatu na Mwenyekiti wake aliteuliwa mwishoni mwa mwaka 2017 na kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka 2020.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Magereza Mkoa wa Rukwa ACP. Simon Ihunja amezitaja changamoto zinazowakumba wafungwa hao wanapotoka gerezani huku kubwa likiwa ni kukosa kuwezeshwa wanapotoka magerezani baada ya kutumikia vifungo vyao.
“Mpango huu huwavutia wafungwa na kuona umuhimu wa kukaa vizuri gerezani ili waweze kutuliwa au kuchaguliwa kumalizia kifungo wakiwa nje, changamoto inayowakumba ni ile ya kwamba wanapotoka wanakuwa hawana kianzio ya kwamba anakwenda kuanza vipi wakati ameshatumikia miaka 10 hadi 15,” Alisema.
Bodi hiyo iliyozinduliwa ni bodi ya sita kutekeleza majukumu yake tangu kuzinduliwa kwa bodi hiyo mara ya kwanza mwaka 2003 na hadi sasa imewanufaisha wafungwa 176 ambapo mmoja wa wafungwa hao alivunja masharti ya bodi hiyo na kukamatwa na kurudishwa tena gerezani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa