Katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanafahamu juu ya namna ya kujikinga na Ugonjwa hatari wa Corona, Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ameanza kuzunguka katika vijiji vya Bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga na kutoa elimu juu ya tahadhari ya ugonjwa huo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ikiwa ni hatua ya kuwataka wananchi hao kuachana na tabia, mila na desturi zitakazochangia kuenea kwa ugonjwa huo endapo utaingia nchini.
Wakati akielezea miongoni mwa mila zinazotumika katika bonde hilo Mh. Wangabo alisema kuwa wakati wa maandalizi ya chakula huletwa maji ya kunawa kwenye bakuli na sufuria na kisha huanza kunawa baba na kufuata Watoto wakubwa hadi wadogo katika chombo hicho ambapo maji humwagwa pale tu yanapobadilika rangi kutokana na uchafu wa mikono hiyo hali ambayo endapo Corona itaingia itasambaa kwa urahisi.
“Lakini mnapoenda makanisani kule, maji ya baraka si yanakuwa pale mwanzoni pale mwa kanisani unapoingia kwenye mlango, unaweka mkono wako pale halafu msalaba(akionesha alama ya msalaba), na mwingine mkono, na mwingine mkono, na mwingine hivyo hivyo, Corona itatumaliza, tuone namna gani ya kufanya hata kwenye maji ya baraka, Wachingaji, Mapadre, mababa paroko wakae watafakari namna gani nzuri ya kutoa maji ya baraka vinginevyo ugonjwa ukiingia utatumaliza,” Alishauri
Na kuongeza kuwa kuna watu wanatabia ya kukohoa bila ya kuziba midomo yao na hivyo kuwaasa kuacha tabia hiyo na kueleza kuwa miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni kusikia homa kali sana, mafua makali na kichwa kuuma na hivyo kuwataka wananchi hao endapo watahisi dalili hizo ni vyema kuwahi kituo cha huduma za afya kuangalia afya yako na kuwaomba kuwaripoti wageni wote wanaoingia kutoka nje ya nchi katika maeneo hayo ya vijiji.
Aidha, amesisitiza wanarukwa kuanza tabia ya kutoshikana mikono jambo ambalo amelieleza kuwa ni gumu sana lakini wananchi hao hawana budi kuanza kujenga mazoea hayo na pia kuacha tabia ya kupokezana pombe katika vilabu vya kienyeji kwani kuna tabia ya wanywaji hao kabla ya kuinywa pombe hiyo huipuliza kwanza na kisha kunywa na kumpatia aliyekaribu yake na hatimae kuizungusha kwa wengine.
“Kwahiyo Desturi zetu ambazo tumezizoea basi tuzibadilishe kila mtu aweke tabia ya kunywa mwenyewe, sio ya kugawana gawana hivyo, mkigawana gawana hivyo mtagawana mengi, mtagawana mpaka na haya magonjwa,magonjwa sasa hivi ni mengi kuliko zamani, zamani magonjwa yalikuwa ni machache lakini sasa hivi ni mabadiliko ya tabia nchi yameleta magonjwa mengi, kwahiyo na sisi tubadilishe Maisha yet una namna ambavyo tumezoea kuishi ili tuweze kuwa salama,” Alisisitiza
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kuzungukia vijiji sita katika kata mbili za bonde la ziwa Rukwa ambazo ziliathirika na mvua iliyoambata na upepo mkali kuangusha nyumba zaidi ya 135 na na kaya zaidi ya 72 kukosa mahala pa kuishi hali ilimpelekea kutoa msaada wa kilo 500 za unga wa sembe pamoja na kilo 200 za maharage kama mkono wa pole kwa familia hizo zilizokubwa na majanga hayo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa