Mkuu wa Mkoa wa rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasisitiza watumishi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Rukwa kufanya kazi kwa ushirikiano pindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata huduma.
Ameyasema hayo alipofanya ziara katika Hospitali hiyo kwa lengo la kujionea ubora wa huduma zinazopatikana katika hospitali hiyo ambapo alipita katika wodi mbalimbali na kuzungumza na wagonjwa kadhaa waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.
“lazima tuwe na “team work” tushirikiane, ili tutatue shida na changamoto kwa haraka zaidi, sisi sio watuwa kuanza kunyoosheana vidole kwanini Fulani hukufanya hivi na vile, ukimwambia mwenzio hivyo wewe mwenyewe ulikuwa wapi, wote mnafanya kazi kwenye hospitali moja, tuambiane mapema ili shida iwe yetu sote na mafanikio yawe yetu sote,” Alisema.
Aidha alisifu juhudi za utoaji huduma zinazofanywa na hospitali hiyo baada ya kusikia kutoka katika midomo ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kuwa hakuna usumbufu wanaoupata na wanahudumiwa vizuri.
Mmoja wa mama mjamzito aliyelazwa katika hospitali hiyo baada ya kufanyiwa upasuaji na kujifungua mtoto Bi. Elizabeth Justin Alisema kuwa tangua afike katika hospitali hiyo amekuwa akihudumiwa bila ya wauguzi kuchoka na kumsikiliza kwa kila shida aliyokuwa akiwaeleza wauguzi hao pamoja na madaktari.
“Tangu nimefika hapa, nimehudumiwa vizuri, nawasifu wauguzi pamoja na madaktari wa hospitali ya Mkoa kwakweli wamenisaidia sana, hakuna changamoto zozote tunazozipata hapa,” Alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa