Sumbawanga, Na Khadija Dalasia
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Msalika Makungu, amepokea ujumbe kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) uliokuja kutambulisha mradi mpya wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi Kelvin Tarimo alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni 291.3 zimetengwa kutekeleza mpango huo katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, ikiwemo Rukwa.
Kwa upande wa Rukwa, jumla ya majiko 5,094 yatasambazwa katika wilaya tatu za Kalambo, Sumbawanga na Nkasi, ambapo kila wilaya itapokea majiko 1,698.
“Mradi huu unalenga kukuza upatikanaji wa nishati safi na endelevu, kupanua matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na afya,” alisema Mhandisi Tarimo.
Amesema kuwa REA imeandaa mpango wa kusambaza majiko banifu 200,000 kwa bei nafuu, ambapo gharama ya jiko moja bila ruzuku ni Shilingi 71,500, lakini kupitia ruzuku ya serikali ya asilimia 80, wananchi watanunua kwa bei ya Shilingi 14,300/=.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya mradi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Msalika Makungu, aliishukuru REA kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Katika Mkoa wa Rukwa, usambazaji na uuzaji wa majiko banifu utafanywa na makampuni ya Greenway Grameen Infra Pvt Limited na ECOMANA Tanzania Limited.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa