Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanapambana na kutokomeza udumavu kwa watoto unaosababishwa na ukosefu wa Lishe bora.
Ameyasema hayo akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua shughuli za utoaji huduma za Afya, na uhamasishaji wa vikundi vidogo vidogo vya wanaweke vya ujasiriamali katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.
”Mkoa wa Rukwa haupaswi kuwa na utapiamlo hata kidogo, asilimia 60 ya udumavu ndani ya Rukwa ni kiasi kikubwa sana, katika mkoa ambao una chakula na ardhi yenye rutuba nzuri ni jambo la kushangaza kuona tatizo hili”, Alisema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile aliendelea kwa kusema kuwa, Siku 100 za mwanzo tangia mtoto anazaliwa ni muhimu na nyeti sana katika kuhakikisha anapata maziwa ndani ya miezi sita, na anapoanza kula ale vyakula vyenye lishe ya kutosha ili ubongo wake ukue vizuri.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa maelekezo kwa sekretarieti ya Mkoa na viongozi wa kisiasa kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu ya kutosha kwenye kila mikusanyiko watakayofanya kuhusiana na masuala ya Lishe bora ili kutokomeza janga hili linalosumbua idadi kubwa ya watoto katika Mkoa huu.
Kwa upande wake Mbunge wa Sumbawanga Mh. Aishi Hilaly amemshukuru Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile kwa kuwakumbuka katika mgao wa fedha za kuboresha Vituo vya Afya cha Mazwi, pia hakusita kupaza sauti juu ya ombi la gari la kubebea wagonjwa litakalosaidia kupunguza hadha kubwa wanayokumbana nayo inayotokana na kukosekana kwa gari hilo.
Nae Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface Kasululu Mkoa unaendelea kupambana na magonjwa ya mlipuko hasa ugonjwa wa kipindupindu kwa kutoa elimu ya Afya na Usafi wa mazingira kwa wananchi, ili kuhakikisha magonjwa haya yanakuwa historia katika mkoa wa Rukwa.
Aidha, Dkt. Kasululu alimuomba Dkt. Faustine kupunguza hadha ya upungufu wa madaktari bingwa na mabingwa wa fani nyingine, Dkt. Kasululu alisema kuwa hadi kufikia Desemba 2017 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa inajumla ya madaktari bingwa 5 ambao ni sawa na asilimia 21 kati ya madaktari 24 wanaohitajika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa