Mkoa wa Rukwa leo tarehe 2.5.2020 umeungana na baadhi ya mikoa mingine katika kutekeleza awamu ya pili ya zoezi la kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura ambapo awamu hii utafanyika katika ngazi ya vituo vya kata ikiwa ni hatua za tahadhari ya kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19)
Hayo yamesemwa na Afisa Serikali za Mitaa Albinus Mgonya wakati akitoa salamu zake katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini, ambapo alisema kuwa zoezi hilo litakamilika tarehe 4.5.2020.
Mgonya alisema kuwa zoezi hilo la kuboresha daftari la kudumu litakwenda sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura waliojiandikisha katika uboreshaji wa awamu ya kwanza na kuongeza kuwa uwekaji wazi huo unapatikana katika vituo vyote ambapo mwananchi alijiandikisha katika vituo vilivyokuwa vimeainishwa na halmashauri.
“Mheshimiwa Mwenyekiti lengo la hatua hii ni kuwapa fursa wananchi waliojiandikisha awali ili waweze kuhakiki taarifa zao, kwa maana ya kwamba kama majina yamekosewa au na taarifa nyingine kadiri itakavyobidi,” Alisema.
Aidha aliwaweka wazi wahusika wa zoezi hilo kuwa ni wananchi waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawakupata fursa ya kujiandikisha awali, watakaotimiza umri wa miaka 18 ifikapo Oktoba, 2020, waliojiandikisha na kuhama kata ama jimbo, wananchi wenye taarifa au majina yaliyokosewa wakati wa uandikishaji, waliopoteza kadi zao ama kuharibika.
Halikadhalika aliweka wazi utaratibu wa kuendesha zoezi hilo kwa kuzingatia hatua zote za kiafya zinazotakiwa kuchukuliwa wakati wa kutekeleza zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kituo kuwa wazi na chenye nafasi ya kutosha ili kutoruhusu msongamano.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa