Mkoa wa Rukwa umejipanga kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kuhakikisha wanatumia rasilimali za makaa ya mawe yanayopatikana katika kijiji cha Nkomolo tu, Wilayani Nkasi kuwa mkaa mbadala na kuanza kutumika majumbani.
Mkakati huo ulioanza kwa mafunzo ya siku mbili yaliyoendeshwa na mtaalamu wa makaa hayo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe bi. Halima Mpita ukiwakutanisha makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, madiwani, wataalamu wa mazingira kutoka katika halmashauri, mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia mazingira pamoja na wazee maarufu.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya nishati mbadala inayotokana na makaa ya mawe mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachima Wangabo amesema kuwa tunafanya kila liwekanalo kuokoa kile kilichopo na kuhakikisha kwamba mazingira hayaendelei kuharibiwa kwa namna yoyote hasa masuala ya kukata miti kwaajili ya kuni na mkaa.
“Makaa ya mawe yapo kilomita 45 toka hapa tulipo (sumbawanga mjini), yale makaa yam awe tunaweza kuyatumia kama mkaa mbadala kwa matumizi ya majumbani, na hili ndio lengo la mafunzo ya leo, mtaalamu wetu atatueleza kule Songwe wanafanyaje, kile wanachofanya kule watatumegea hapa uzoefu wao, na sisi tutaona na kujipanga tufanye nini na haya makaa yam awe tuliyonayo,” Alisema.
Ameongeza kuwa endapo mafanikio yatapatikana na kuanza kutumia makaa ya mawe majumbani, kiwango kikubwa cha uvunaji wa miti kitaokolewa na kutahadharisha kuwa mpango huo ukifanikiwa gharama za kununua bidhaa hiyo isiwakatishe tamaa wanunuzi ili wasirudi tena kukata miti na hatimae kutofikia lengo.
Kwa upande wake Bi. Mpita alisifu muitikio wa wadau wa mazingira wa mkoa wa Rukwa na kusema kuwa endapo nguvu hiyo itafikisha elimu kwa wananchi basi mkoa wa Rukwa utakuwa wa kuigwa na kuongeza kuwa atashirikiana bega kwa bega ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.
Akieleza faida za mkaa unaozalishwa na makaa yam awe alisema, “Haya makaa ni suluhisho la kudumu juu ya matumizi mbadala la mkaa wa miti kwa kuwa miamba ya makaa ya mawe ni ya asili na inaweza kuvunwa zaidi ya miaka 500. Pia unaweza kuwaka kwa saa 3 hadi 4 mfululizo na hautoboi wala kuchafua sufuria, ni mkombozi wa ajira maana uanzishaji wa kiwanda chake ni rahisi na majivu yake hustawisha mimea,” Alisisitiza.
Ili kuuwasha Mkaa wa makaa ya mawe unahitaji jiko la mkaa lililotengenezwa kwa udongo, utawasha vijiti viwili maalum vya kuwashia moto utaweka vipande 4 hadi 5 acha viwake pamoja kwa dakika 3, ongeza mkaa na uache uko kwa dakia 15 hadi makaa ubadilike na kuwa rangi nyekundu kuanzia chini. Vipande 34 vya mkaa vinatosha kumaliza mapishi ambapo mkaa huo huwaka kwa masaa 3 hadi 4.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa