Sumbawanga,13 Mei 2025.
Mkoa wa Rukwa umeanza rasmi utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani. Katika hatua za awali, katika msimu wa Mwaka 2024/2025 mfumo huo utahusisha zao la mbaazi na ufuta.
Maelezo hayo yametolewa leo Mei 13, 2025 na Mheshimiwa Nyakia Ally Chirukile Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga alipomwakilisha Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa katika kikao cha Maandalizi ya Msimu wa Masoko ya Mazao kwa Mwaka 2025/2026.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Sumbawanga ameeleza kuwa hatua hiyo ya Serikali inalenga kusaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao na bei zenye tija.
Akifafanua juu ya matumizi ya mfumo huyo Mheshimiwa Chirukile ameeleza kuwa kuanzia msimu wa Mwaka 2024/2025, mazao ya mbaazi na ufuta hayatasafirishwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine pasipo kuthibitisha kuwa yalipatikana kupitia minada ya kidigitali ya stakabadhi ghalani.
Ametoa mfano wa Mikoa ya Lindi na Ruvuma ambako mfumo huo umekuwa ukitumika na kuleta mafanikio. Amewahamasisha wakulima wa Mkoa wa Rukwa kuutumia mfumo huo kwa manufaa yao na sekta ya kilimo kwa ujumla.
Aidha Mheshimiwa Chirukile amewataka viongozi wa Halmashauri, Vyama vya Msingi (AMCOS), pamoja na taasisi wezeshi kama TMX, COPRA na WRRB kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mfumo huo ili kuimarisha usimamizi wa soko na ubora wa mazao.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa RDC ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na kuhudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Seksheni kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Vyama vya Ushirika na Taasisi Binafsi na Wakulima.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa