Na Khadija Dalasia - Kalambo, Rukwa.
Katika juhudi za kuimarisha afya ya uzazi na kulinda maisha ya mama na mtoto, Mkoa wa Rukwa umeanza kikao kazi cha siku mbili kinacholenga kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na changamoto za huduma kwa watoto wachanga.
Kikao hicho kimefunguliwa Julai 28, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo. Kimewakutanisha wataalamu wa afya kutoka ngazi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo wanaoshiriki katika sekta ya afya ya uzazi.
Katika kipindi cha Machi 2021 hadi Juni 2025, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 20.9 kwa Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto. Fedha hizo zimetumika kujenga hospitali mpya 4 za wilaya, kuboresha vituo vya afya 11, kukamilisha zahanati 13 na kujenga nyumba za watumishi wa afya.
Mkuu wa Mkoa ameagiza kila kifo kinachotokana na uzazi kuchunguzwa kwa mujibu wa miongozo ya kitaifa, kuwepo kwa bajeti mahsusi ya afya ya uzazi kila mwaka, kuimarisha huduma za dharura, kusimamia mifumo ya rufaa kwa weledi, na kuhakikisha ajenda ya mama na mtoto inajadiliwa kwenye mikutano ya kijamii.
Pia ametoa wito kwa wadau wa afya kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa vifaa tiba, kutoa mafunzo kwa watumishi na kuongeza motisha kwa watoa huduma waliopo vijijini.
Kikao hiki ni sehemu ya juhudi za Mkoa wa Rukwa kuleta mageuzi katika huduma za afya ya uzazi na kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa