Sumbawanga.
Leo Julai 24, 2025 Mkoa wa Rukwa umefanya kikao muhimu cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), kikiwa na lengo la kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8 wanapata huduma bora katika hatua za awali za maisha yao.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (RDC) na kuongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Salehe Msanda, ambaye amezitaka Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Rukwa kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu afua mbalimbali zinazolenga maendeleo ya awali ya mtoto.
Katika hotuba yake, Bw. Msanda amesisitiza kuwa mafanikio ya Programu hiyo yanategemea kuwepo kwa mikakati madhubuti inayotekelezeka, inayopimika na inayoleta ushirikiano kutoka sekta mbalimbali.
Aidha, amezitaka Halmashauri kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, ili kuhakikisha kwamba kila mtoto katika Mkoa wa Rukwa anapata huduma stahiki zinazochangia ukuaji na maendeleo yake ya kimwili, kiakili, kijamii na kihisia.
Afua tano kuu zinazounda msingi wa maendeleo ya awali ya mtoto zimejadiliwa katika kikao hicho. Afua hizo ni afya bora, lishe ya kutosha, malezi yenye muitikio chanya, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama wa mtoto
Washiriki wa kikao wametoka katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali, jambo linaloonesha mshikamano wa kijamii katika kutekeleza ajenda ya mtoto.
Serikali ya Mkoa wa Rukwa inaendelea kujizatiti kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata fursa ya makuzi bora tangu akiwa mchanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwekeza katika kizazi chenye afya, maarifa na maadili kwa maendeleo ya Taifa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa